NA FAUZIA MUSSA
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka viongozi wa Wizara ya Afya kusimamia kwa ukaribu uwendeshaji wa mitambo ya hewa tiba ( oxygen plants) ili idumu kwa muda mrefu kwa maslahi ya sasa na kizazi kijacho.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na watendaji hao wakati wa ufunguzi wa mitambo hiyo katika hospital ya rufaa ya Mkoa wa Mjini magharibi -Lumumba.
Aidha Hemed aliwataka viongozi hao kutosita kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya uzembe unaosababisha uharibifu wa mitambo hiyo.
Vilevile Hemed aliwataka watendaji watakaopewa jukumu la kuendesha mitambo hiyo, kuitunza na kuifanyia matengenezo kwa wakati uliowekwa na kuitumia kwa uangalifu kulingana na maelekezo sahihi ya utumiaji wa mitambo hiyo.
Alifahamisha kuwa kupatikana kwa mitambo hiyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuondoa kadhia na usumbufu uliokua ukijitokeza kabla.
Alisema huduma hiyo mbali na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa lakini pia itapunguza gharama za ununuzi wa hewa tiba kama ilivyokuwa hapo awali.
Alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kuelekea kutimiza malengo ya kutimiza dira ya maendeleo endelevu ya Zanzibar 2050, ambayo inalenga kudumisha mfumo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote zitakazotolewa na wataalamu bingwa kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa.
Mbali na hayo Hemed aliwakumbusha wananchi kuendelea kuitumia hospital ya Lumumba kwa kufuata utaratibu wa rufaa kama miongozo ya Wizara ya afya ilivyoelekeza.
Wakati huo huo Hemed aliwashukuru watendaji wa mfuko wa Dunia wa kupambana na malaria Ukimwi na Kifua kikuu (Global Fund) kwa jitahada zao katika kupatika huduma hiyo inayokwenda sambamba na maelekezo ya Shirika la afya ulimwenguni (WHO).
Kwa upande wake Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazurui, aliwataka watoa huduma kuthamini juhudi za Serikali kwa kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kusaidia huduma za matibau kwa mda mrefu.
Alisema matarajio ya Wizara ya Afya ni kuwa mtambo huo utakuwa chachu ya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa nguvu mpya, kasi na ari ya kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Alifahamisha kuwa awali upatikanaji wa hewa tiba haukuwa wa uhakika na kulazimika kwa nyakati tafauti kununua tiba hiyo kutoka Tanzania Bara au katika sekta binafsi zilizopo nchini jambo ambalo liliigharimu Serikali na kurudisha nyuma juhudi za watoa huduma hiyo.
Hivyo hatua hiyo itasaidia kuuzalishwa na kusambazwa kwa hewa tiba katika hospitali mbalimbali za serikali na binafsi na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na yakisasa zaidi.
Mazrui alisema kuwa wakandarasi na wafanyakazi watakaotumia na kuhudumia mitambo hiyo watapatiwa mafunzo ya matumizi na njia bora ya utunzaji wa mitambo hiyo, ili kudumu na kutumika kwa muda mrefu.
Akitoa Taarifa ya kitaalamu Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo Amour Suleiman Mohammed alisema mitambo hiyo miwili imegharimu Jumla ya Dola za Kimarekani 104,880, ambapo (12%) ni mchango kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Jumla ya Dola za Kimarekani 866,279.32 zimetumika hadi kukamilika kwa uwekaji wa mitambo hii pamoja na vifaa vyake, Dola za Kimarekani 52,140.88 ilitumika kwa ajili ya ununuzi wa Jenerata la dharura, (Emargency generator), Dola za Kimarekani 18,630.13 zililipwa kuunganisha umeme wa Taifa, Dola za Kimarekani 339,360 zilitumika kwa utengenezaji wa kitako na banda la kuwekea Mitambo hii (Slab construction) uliojengwa na kampuni ya LEAD BELL ya Tanzania.” Alifafanua Mkuu huyo
Alifahamisha kuwa Mtambo Mkubwa wa kwanza katika mradi huo una uwezo wa kuzalisha oxygen 40 meter cube kwa saa ambao utaunganishwa na mnyororo wa Hewa tiba (Piped system) iliyounganishwa moja kwa moja katika wodi za kulaza wagonjwa, vyumba vya upasuaji (Theater) chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), chumba cha wagonjwa wa dharura (Emergency) na kuwezesha wagonjwa kuwekewa Hewa tiba moja kwa moja kutokea kwenye vitanda vyao.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa mtambo mdogo wa pili una uwezo wa kuzalisha 20-meter cube kwa saa ambapo mtambo huo utatumika kujaza oxygen katika mitungi itakayosambazwa katika hospitali mbalimbali za Wilaya Unguja na Pemba.
“ mtambo huu ndani ya saa 12 una uwezo wa kujaza mitungi 32 hadi 40 ikiwa tayari kusambazwa katika hospitali nyengine.”
Naye Mwakilishi wa Mfuko wa Dunia (Global Fund), Dk. Sara
Asiimwe, alisema Taasisi hiyo itaendelea kusimamia mataengenezo ya mitambo hiyo kwa kipindia cha miaka mitano toka kukabidhiwa kwake.
Aidha alisema global Fund itaendeleza mashiikiano yake na Zanzibar katika kupambana na Ukimwi, maleria na kifua kikuu.
Mbali na kuzinduliwa mradi huo katika Hospitali ya Mkoa wa Mjini –Lumumba mitambo mengine ya kuzalishiwa hewa tiba imejengwa katika Hospitali ya rufaa Mnazimmoja, hospitali Wilaya Mwera Pongwe kwa upande wa Ungua na Vitongoji kwa upande wa Pemba na kuifanya Zanzibar kuwa na vituo vinne vya mitambo hiyo.

