Na,Nishan khamis
Zanzibar.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Paul, ameitaka jamii kuelewa kuwa mtoto wa kike ana haki ya kushiriki michezo yote bila kudhalilishwa. Ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani, yaliyoandaliwa na wadau wa michezo kwa maendeleo Zanzibar, wakiwemo Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na shirika la Ujerumani (GIZ), katika viwanja vya Mau Zi Dong, Kikwajuni. Maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha ushiriki wa watoto wa kike na ustawi wa kijinsia katika michezo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Anna amesema jinsia zote zina haki sawa ya kushiriki michezo, na jamii inapaswa kutambua uwezo wa watoto wa kike na mchango wao katika jamii. Alisisitiza kuwa ni jukumu la jamii kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ukatili wa kijinsia, akiwa katika mazingira yoyote. Aidha, alieleza kuwa michezo inawasaidia watoto wa kike kujenga afya zao za kimwili, kiakili, kukuza ushirikiano, na kuwawezesha kufurahi kwa pamoja.
"Michezo inamuwezesha mtoto kufaulu vizuri iwapo hatopuuzia masomo yake, kwani inaondoa fikra mbaya," alisema Mhe. Anna. Pia aliongeza kuwa kuna haja ya kuwaongezea watoto wa kike ujuzi katika masuala ya uongozi na ushirikiano, na kuwawezesha kuchukua nafasi kubwa zaidi katika uongozi wa jamii.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), Hashim Pondeza, alisema kuwa wanahamasisha jamii kufahamu umuhimu wa kumpa mtoto wa kike kipaumbele kushiriki kwenye michezo mbalimbali. Alisisitiza kuwa usalama wa mtoto wa kike utahakikishwa pamoja na kuheshimu mila na desturi za jamii. "Mtoto wa kike akishiriki michezo anapaswa kuvaa nguo za stara kama hijabu," alisema Pondeza.
Mwalimu wa Skuli ya Bububu, Bimkubwa Abdurahman Ame, alisema kuwa michezo inawasaidia watoto wa kike kujichanganya na makundi tofauti, kubadilishana mawazo, na kutoa fursa za ajira.
Nao wanafunzi walioshiriki mchezo wa netball, Zubeda Said Ali na Ibrahimu Kamis Haji kutoka Kianga, walieleza furaha yao ya kushiriki michezo, wakisema kuwa wanapata uzoefu mpya wa kucheza michezo ambayo hapo awali hawakushiriki, kama vile mpira wa miguu.

