Na, Khamis Nishan.
Zanzibar:
Katika mazingira ya elimu ya juu, wasichana wanapata fursa ya kujifunza na kujiimarisha katika uongozi, kama anavyodhihirisha Najla Abdalla Musa, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar - IPA, Najla anachukua shahada ya mahusiano ya kimataifa na diplomasia ndio msichana wa kwanza kuwa mwanamke wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, ambacho kilianzishwa rasmi mwaka 2007.
Safari ya kugombea urais haikuwa rahisi, Najla alikabiliana na changamoto za udhalilishaji wa kijinsia na ubaguzi, hali iliyomfanya afikie hatua ya kutaka kujiondoa kwenye kinyang’anyiro. "Wengine walisema 'si ukapike tu nyumbani!', lakini kwa msaada wa wazazi wangu, walimu, na baadhi ya wanafunzi wenzangu, nilipata nguvu ya kuendelea na uchaguzi na nilishinda" Amesema na kuendelea kueleza kuwa mitaala ya chuo hicho imemjenga, ikimfundisha mbinu za kutatua migogoro, kujenga taasisi, na kuimarisha ujasiri wake. "Kutokana na masomo tunayojifunza, tumefundishwa namna ya kushiriki vikao na kushughulikia changamoto za taasisi kwa ufanisi," Anakiri Naijal ambaye kwa sasa ni kiongozi.
Najla Abdalla Musa, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo cha Utawala wa Umma(IPA)
Ndoto zake haijaishia hapo ila atahesabu mafanikio yake pale atakapobahatika ni kuingia katika baraza la chuo, ambalo wasimamizi wake huteuliwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwakilisha maslahi ya wanafunzi wenzake, hususani wasichana.” Hapa nitaona mafanikio na nitawakilisha sauti za wanawake” Amemaliza Naijal.
Time Sharif Suleiman ni mwanafunzi anayesoma Chuo kimoja nma Najla,yeye anaamini kwamba mitaala ya elimu ya juu inawajenga wanafunzi kujiamini zaidi na kufuatilia fursa za uongozi, "Mimi sisomi moja kwa moja masomo ya uongozi lakini kupitia somo la uongozi lile somo limenijenga kwa kiasi kuja kuwa kiongozi kama mwanamke na naamini hilo linawezekana" Amesema Time.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inatoa fursa sawa ya ushiriki wa wanawake na wanaume katika nyanja zote za maisha. Sura ya 3 Ibara ya 12(2) ya Katiba inatoa haki ya kuheshimiwa kama ilivyoainishwa katika tamko la kimataifa la haki za ninadamu. Vilevile, Ibara ya 21 ya Katiba inasisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kushiriki katika uongozi moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi, ambapo Ibara ya 22 inatoa fursa sawa za kushika madaraka ya Umma.
Jumla ya wanafunzi wa elimu ya juu 8,161 waliomba mkopo wa kusoma elimu ya juu kwa mwaka 2023/2044 huku katia ya hao 5,900 walipata ambao wanaume walikuwa 1,114 na wanawake walikuwa 1,151.
Katika Chuo Cha Kumbu kumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Zanzibar, Zainab Juma Ali, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika shahada ya jinsia na maendeleo. Zainab amesema kuwa mitaala ya elimu ya juu inawaandaa vyema wanawake kuwa viongozi. "Suala la usawa wa kijinsia linalindwa sana chuoni, ingawa bado tunakosa msaada wa kutosha kutoka kwa baadhi ya watu ila masomo yanatusaidia," Amebainisha Zainab.
Makame Khamiss Makame, Mwenyekiti wa Shirikisho la Elimu ya Juu Zanzibar, amesema kuwa mitaala ya elimu ya juu imebuniwa kuwaandaa wanafunzi, wakike na wakiume, kuwa viongozi bora katika ngazi mbalimbali.”Zahalife sisi katiba yetu ya 2013 tumeweka kipaumbele kwa wanawake mfano kifungu cha 13(1e) ukurasa 15 nafasi za wajumbe ni 5 katika nafasi hizo tatu ni wanawake na mbili ni wanaume" Amesema Makame wakati akifafanua jinsi wanavyotoa nafasi kwa wanawake.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Elimu ya Juu Zanzibar Makame Khamis Makame.
Chapisho la Wizara ya Elimu Zanzibar tarehe 28 disemba 2023 linaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi wa kike walioandikishwa katika taasisi za elimu ya juu imeongezeka kwa asilimia 31 kati ya mwaka 2019 na 2023, ikiwa ni dalili nzuri ya maendeleo ya elimu kwa wanawake. Hata hivyo, changamoto ya kuwajenga wanawake kuwa viongozi bado inahitaji kutiliwa mkazo zaidi.
Mussa Mustafa Twalib, ni Mkufunzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar - IPA, amesema kuwa mitaala ya chuo hicho imekuwa na nafasi kubwa katika kuwajenga wanawake kuwa viongozi.”Uwepo wa dawati la jinsia hapa chuoni limesaidia kwa kiasi kikubwa kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike kwani hushirikiana katika kuelimisha na kusaidia masuala yanaweza kusimama na kusimamia mambo yao” Amesema Mussa.
Licha ya maendeleo haya, Abdallah Hijja, Mwanaharakati wa masuala ya vijana Zanzibar, anaamini kuwa bado mitaala ya elimu haiwaandai vya kutosha wanawake kuwa viongozi, badala yake inawajenga zaidi kuwa wafanyakazi, "Mimi naona asilimia 40 ndio wasichana waandaliwa kuwa viongozi lakini asilimia 60 hawaandaliwi kuja kuwaongoza wengine bali asilimia kubwa wanaandaliwa kuwa viongozi na kutafuta ajira elimu yao" Amesema Abdallah huku akitaka mitaala hiyo kuwekewa mkazi wa masomo ya uongozi kwa wanawake.
Najla amewataka wanawake waliopo vyuoni kusimama na kuthubutu ili waweze kuwa viongozi kwenye ngazi hizo na baadae kuja kugombea kwenye sehemu za maamuzi” Tukianza huku chini vyuoni na huko mbele tutaweza na tutafanikiwa” Amehitimisha Naijal.

