Na - Khamis Nishan.
Zanzibar:Mitandao ya kijamii imeleta mapinduzi makubwa katika mawasiliano kwa sasa hususani kwenye masuala kisasa, ikitoa fursa za kipekee kwa viongozi, wakiwemo wanawake, kujitangaza, kujenga majukwaa ya kuwasiliana na jamii, na kushawishi sera za kisiasa. Hata hivyo, pamoja na fursa hizo, changamoto mbalimbali zinawakabili wanawake viongozi juu ya matumizi ya mitandao.
Siti Ali Makame 55, alianza siasa rasmi mwaka 2024, ni Diwani wa Wadi ya Bandakuu Nungwi wilaya ya kaskazini A Unguja mkoa wa kaskazini Unguja , amesema licha ya maendeleo ya kidijitali, si mara kwa mara anatumia mitandao ya kijamii katika shughuli zake za uongozi. Ameeleza kuwa mtandao anaoutumia kwa kiasi kidogo ni WhatsApp pekee, ingawa ana hamu ya kujifunza zaidi juu ya mitandao mingine ili aitumie katika harakati zake za kisiasa na kijamii."Mara moja moja sana natumia WhatsApp katika magroup nyumbani. Najua ni fursa nzuri ya kujitangaza juu ya harakati zangu, ila sipati watu wa kunipa elimu ya mitandao. Watuone na sisi watu wa vijijini kujua juu ya kutumia fursa hizi," Amesema Siti huku akiwa na shauku ya kupata elimu sahihi ya matumizi ya mitandao, ataweza kuzifuata fursa hizo na kuwa na njia rahisi ya kuonesha uwezo wake wa uongozi kupitia mitandao.
Chapisho la Women at Web Tanzania la Januari 17, 2022, linaeleza kuwa takriban asilimia 77 ya wanawake wanaojihusisha na siasa nchini Tanzania wamesimamisha kwa muda matumizi ya mitandao ya kijamii kutokana na unyanyasaji wa kijinsia.Chapisho hilo limeeleza kuwa aina kubwa ya unyanyasaji ambao wanawake wanasiasa wamezitaja ni uchokozi wa mtandaoni asilimia 77,kukera kwa makusudi asilimia 61, kuvunjia heshima asilimia 47, na udhalilishaji wa kimwili asilimia 43.
Utafiti huo ulionesha kuwa asilimia 73.1 ya wanawake waliohojiwa walikiri kutokuwa na mafunzo ya kuwasaidia kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, huku asilimia 76.9 wakiwa tayari kupatiwa mafunzo sahihi ya mitandao.
Tunu Juma Kondo ni Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania-UWT Zanzibar,sera ya UWT ni kumuinua mwanamke kisiasa, kiuchumi na kijamiii hivyo anaamini fursa za mitandao ya kijamii ni sehemu sahihi ya kutumia na kuweza kufikia malengo kwa wanawake katika nyanza zote za kiuongozi,kisiasa,kijamii na kiuchumi."Mimi binafsi natumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wanawake kujiingiza katika nafasi za uongozi pale wakati unapofika,Pia tunafanya mengi kupitia mitandao, na sasa watu wengi wanafuatilia mitandao kuliko TV na redio hivyo tunaendelea kuhimiza wanawake viongozi wakimbilie fursa za kidigitali zaidi kwani watu wengi sasahivi wanatumia mitandao kama ni fursa ya kutanua wigo wa kimaendeleo katika kisiasa, kiuchumina kijamiii," Amesema Tunu huku akitamani kuona mabadiliko ya matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuogeza wigo kwenye nafasi za uongozi.
Kwa Mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, lilieleza kuwa wanawake hukumbana zaidi na unyanyasaji wa kimtandao kuliko wanaume. Kwa takwimu za Marekani, watu 30 huripotiwa kufa kila siku kutokana na udhalilishaji na ukatili wa kimtandao yaani Cyber Bullying.Bunge la Tanzania mwaka 2015 lilipitisha Sheria ya Makosa ya Kimtandao, ambapo vifungu vya 13 na 14 vinazuia uchapishaji wa picha za ngono ponografia zinazohusisha watoto na unyanyasaji kupitia mitandao.
Nasra Nassor Omar, Naibu Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje kupitia Chama cha ACT-WAZALENDO, amesema kuwa licha ya changamoto za unyanyasaji wa kimtandao, mitandao ni sehemu sahihi kwa wanawake kuzikimbilia fursa mbalimbali zitakazowawezesha kujinufaisha kiuchumi na kijamii na hata kwenye uwanja wa kisiasa."Mimi pia ni mfanyabiashara,natumia mitandao ya kijamii kwa wateja wangu wengi,nawapata kupitia mitandao. Pia chama chetu kipo vizuri katika matumizi ya mitandao, na tunahamasisha wanachama wetu kuitumia kwa ajili ya ushawishi katika harakati za kisiasa, kijamii, na kiuchumi," Amesemea Nasra.
Labda suala ya mitandao ya kijamii ni suala ambalo bado linazungumzwa zaidi kama fursa ya kibiashara ila ushawishi wa majukwaa hayo kwenye siasa unaweza kuwasaidia wanawake.Suleiman Abdulla ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar -ZBC, amesema kuwa kuelekea kipindi cha Uchaguzi mkuu wa 2025, mitandao ya kijamii ni sehemu sahihi kwa wanawake viongozi kujijenga kisiasa na kujitangaza kwa matumizi sahihi."Mitandao ya kijamii ni sehemu sahihi kwa wanawake kujitangaza.Hata sisi katika kuleta usawa wa kijinsia, kwa kushirikiana na TAMWA-Zanzibar, tunafanya kazi kuhamasisha usawa wa kijinsia katika vyombo vya habari.Amesema Suleiman.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Tanzania, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, kupitia taarifa ya tarehe 9 Disemba 2023, ameleza kuwa watanzania wapatao milioni 34.4 hadi sasa wanatumia intaneti, Takwimu hizo zilionesha kuwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini wamefika milioni 16.7.
Dkt. Mzuri Issa, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania -TAMWA-ZANZIBAR, amesema ukatili wa kimtandao ni miongoni mwa udhalilishaji ambao umekuwa ukiwazuia baadhi ya wanawake viongozi kushiriki kikamilifu katika siasa kwa kuhofia unyanyasaji."Watu washindane kwa hoja na sio kudhalilishana, huku suala la ushawishi la matumizi ya mitandao liwe suala mtambuka kwenye suala hili," Dkt. Mzuri amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yatasaidia kuepusha wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni na kuhakikisha mitandao haitumiwi kueneza vitendo viovu bali kuwa uwanja wa kukuza mijadala ya kuchochea maendeleo.
