Popular services

WAZIRI SORAGA ATOA UJUMBE MZITO KWA VIJANA KATIKA KONGAMANO LA KITAIFA VIJANAWAITIKA.

  

Na Nishan Khamis, Zanzibar
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga, amewataka vijana kutumia vyema majukwaa ya makongamano kama fursa ya kujifunza wajibu wao wa kuwa wazalendo wa kweli na kulinda amani ya nchi, sambamba na kutokukubali kushawishiwa kuunga mkono vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

Waziri Soraga amesema vijana wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walionao kuilinda amani ya nchi kwa maslahi ya sasa na ya baadaye, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya Taifa.
Amesema uwajibikaji wa vijana unapaswa kudhihirisha wazi utayari wao wa kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kwani makongamano hayo hutoa fursa ya kujifunza historia ya Mapinduzi, kuimarisha uzalendo na kuwaandaa vijana kuwa tayari kushiriki katika kulinda na kuendeleza misingi ya Mapinduzi hayo.

Akizungumza katika Kongamano la Taifa la Vijana kuelekea Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lililofanyika katika ukumbi wa New Amani Hotel, Waziri Soraga amesema Serikali imejipanga kutoa ajira takribani laki tatu na nusu, pamoja na mikopo yenye masharti nafuu, kuwajengea vijana uwezo wa matumizi sahihi ya TEHAMA, na kuhakikisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Salama Mbarouk Khatib, amesema uwepo wa wizara hiyo ni dhamira ya kuendesha maendeleo kwa kasi kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa. Amesema wizara ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kuwasaidia vijana wa Zanzibar kupata fursa za ajira ndani na nje ya nchi, sambamba na kuwapatia ujuzi na maarifa muhimu.

Ameeleza kuwa wizara inapaswa kuwa na sera madhubuti zitakazoratibu maendeleo ya vijana ili waweze kufikia malengo yao, kwa kuandaliwa vyema kuwa viongozi na wasimamizi wa Taifa kupitia mada mbalimbali zinazowasilishwa katika makongamano kama hayo.

Kongamano hilo la vijana, lililobeba kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar “Amani na Maendeleo ndio Msingi wa Maisha Yetu”, limewashirikisha vijana kutoka wilaya zote 11 za Zanzibar ambapo baadhi ya vijana wamesema wamefurahishwa na kongamano hilo na kuahidi kuzingatia na kuyafanyia kazi yale yote yaliyo elezwa kaa maslahi yao na taifa kwa ujumla.