Popular services

WAZIRI SHAABAN: FURSA ZA VIJANA KUPITIA BARAZA LA SHEHIA, VIKWAZO VYA MIKOPO KUSHUGHULIKIWA

 

Na Nishan Khamis, Zanzibar.
Jumapili, 21 -12-2025.
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi Zanzibar, Mheshimiwa Shaaban Ali Othman, amewahakikishia vijana kuwa fursa zote zinazohusu maendeleo yao zitapitia Baraza la Vijana kuanzia ngazi ya shehia, huku akitoa ahadi ya kushughulikia vikwazo vinavyowakabili vijana katika upatikanaji wa mikopo.

Akizungumza katika kikao cha vijana kilichofanyika katika Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mheshimiwa Shaaban amesema kikao hicho kililenga kujitambulisha viongozi wa wizara na kukutana na viongozi wa mabaraza ya vijana, ikiwa ni hatua ya kuimarisha maendeleo ya mabaraza hayo kwa ustawi wa vijana nchini.

Amesema wizara yake itahakikisha fursa mbalimbali zinazotolewa kwa vijana zinawafikia kupitia mabaraza ya vijana kuanzia ngazi ya shehia, wilaya, mkoa hadi taifa, na hivyo kuwataka viongozi kuhamasisha vijana kujiunga na mabaraza hayo, kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii. Aidha, ametangaza kuondolewa kwa ada zote za kujiunga na mabaraza ya vijana ili kuongeza idadi ya wanachama.

Mheshimiwa Shaaban pia amewahakikishia vijana kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wa mabaraza ya vijana utakuwa wa wazi, huru na wa haki, na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato huo ili kupata viongozi imara watakaosimamia maendeleo ya vijana nchini.

Kuhusu changamoto ya mikopo kwa vijana, Waziri Shaaban amesema wizara yake inalitambua tatizo hilo na akaahidi kushughulikia vikwazo vya masharti ya mikopo ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameanzisha wizara hiyo kwa dhamira ya dhati ya kutatua changamoto zinazowakabili vijana, na hivyo kuwataka vijana kutunza afya zao, kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi ya kipaumbele yenye tija.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi, salma Mbarouk Khatib, amesema mabaraza ya vijana yapo kikatiba, akisisitiza kuwa maendeleo ya Zanzibar yatapatikana kupitia nguvu na mchango wa vijana. Amesema wizara itahakikisha fursa zilizopo nchini zinawafikia vijana ipasavyo.

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wote wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi Zanzibar, wenyekiti wa mabaraza ya vijana ya wilaya, pamoja na wenyekiti wa mabaraza ya vijana ngazi ya shehia na makatibu wao, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na ufanisi wa mabaraza hayo katika kusukuma mbele maendeleo ya vijana nchini.

Nao baadhi ya vijana waliohudhuria kikao hicho wamempongeza Mheshimiwa Waziri kwa mkutano huo, huku wakieleza kuwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na ukosefu wa ushirikiano wa kiutendaji katika ngazi mbalimbali, ukosefu wa fursa na uhaba wa elimu ya uongozi, hali inayokwamisha maendeleo ya vijana nchini.