Popular services

BARAZA LA UWT KASKAZINI UNGUJA LAKETI KIKAO CHA KIKATIBA, DKT KHALID ATOA WITO WA UMOJA

 

Na Nishan Khamis, Mahonda

Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kaskazini Unguja limeketi kikao chake cha kikatiba huku likitakiwa kuendeleza umoja na mshikamano ili kuimarisha maendeleo ya jumuiya hiyo pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo katika Chuo cha Wajasiriamali UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mahonda, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa wa CCM, Dkt. Khalid Salum Mohamed, wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la UWT Mkoa huo katika kikao hicho cha kikatiba kilicholenga kujadili mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka huu pamoja na changamoto zinazokikabili chama na jumuiya hiyo.

Dkt. Khalid amesema kuwepo kwa makundi ndani ya chama kunarejesha nyuma maendeleo, akisisitiza kuwa UWT ni jeshi kubwa la maendeleo nchini, hivyo ni vyema wanawake kuendelea kushirikiana, kushikamana na kuwaunga mkono viongozi wote waliochaguliwa kwa maslahi ya jumuiya, chama na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa wakati wa makundi umepita na sasa ni wakati wa kuwa pamoja, akiwataka wanawake hao kuandaa mikakati madhubuti ya maendeleo na kuendelea kuhubiri amani na utulivu nchini. Aidha, amewahakikishia ushirikiano wake katika kuimarisha jumuiya zote za CCM ili chama kiendelee kushika dola.

Awali, akisoma ripoti fupi ya utekelezaji wa shughuli za UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kaimu Katibu wa UWT Mkoa huo, Mtenge Makame Faki, amesema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa mwaka huu ni ushindi wa kishindo kwa marais wote pamoja na uwepo wa wabunge, wawakilishi na madiwani wanaotokana na jumuiya hiyo.

Hata hivyo, amesema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukosefu wa nyumba ya Katibu wa UWT Mkoa, pamoja na upungufu wa vitendea kazi vya ofisi kama kompyuta na mashine ya fotokopi.

Akitoa neno la shukrani, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Shadya Haji Omar, amempongeza mgeni rasmi kwa nasaha na maelekezo muhimu aliyoyatoa, akiahidi kuwa UWT Mkoa itayachukua na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuimarisha jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.