Popular services

JUVIEKA YAWAHIMIZA VIJANA KUFANYA UTETEZI NA USHAWISHI WA MAENDELEO NCHINI

 

Na Nishan Khamis, Mkwajuni

Vijana wa Mkoa wa Kaskazini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya utetezi, ushawishi, ushiriki na ushirikishwaji katika harakati mbalimbali za maendeleo pamoja na mabadiliko ya sera, kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini “A” (JUVIEKA) wakati akizungumza katika mafunzo kwa vijana yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Walimu Mkwajuni. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kufanya utetezi katika sera mbalimbali, ushawishi wa kimaendeleo kuanzia ngazi za chini hadi taifa, pamoja na kuhimiza ushiriki wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo nchini.

Amesema kuwa ushirikiano na kupaza sauti kwa pamoja miongoni mwa vijana ni njia muhimu ya kukabiliana na changamoto zinazozikabili jamii, zikiwemo vitendo vya udhalilishaji, unyanyasaji, wizi, ukosefu wa ajira pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imetambua mchango na umuhimu wa vijana kwa kuanzisha Wizara maalum ya Vijana. Hivyo, amewahimiza vijana kutumia fursa hiyo kikamilifu kwa kutoa maoni yao, kushiriki katika vikao vya shehia na kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo kuanzia ngazi ya shehia hadi taifa.

Kwa upande wao, washiriki wa mjadala huo wameishukuru JUVIEKA kwa kuandaa mjadala wenye tija unaolenga kuleta mabadiliko chanya kwa vijana wa mkoa huo. Hata hivyo, wamesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa ajira.

Vilevile, wamesema licha ya kuwepo kwa fursa nyingi za utalii katika mkoa huo, bado jamii ina dhana potofu kuwa sekta ya utalii haiendani na mila na silka za Kizanzibari, hali inayowafanya vijana wengi kushindwa kutumia fursa hizo. Kutokana na hilo, wameiomba serikali kuandaa sera na kanuni bora zitakazowezesha vijana kunufaika na sekta ya utalii kwa kuzingatia maadili ya Kizanzibari.

Mjadala huo umeandaliwa na JUVIEKA kwa kushirikiana na Shirika la ActionAid Zanzibar kwa lengo la kuchochea mabadiliko ya maendeleo nchini.