Popular services

MHE. HEMED AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA TUMBATU, ASISITIZA AJIRA KIPAUMBELE KWA WATUMBATU


Na Nishan Khamis – Tumbatu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu kutaongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya za msingi ikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za dharura, maabara pamoja na huduma za kinga na tiba.

Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu, hafla iliyofanyika ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema uamuzi wa Serikali wa kujenga kituo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na katika mazingira bora yanayozingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hususan kwa maeneo ya visiwa.

Makamu wa Pili wa Rais ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya afya ikiwemo mfumo wa rufaa, ambapo hospitali za wilaya tayari zimekamilika na zinaendelea kutoa huduma kwa wananchi katika wilaya zote za Zanzibar.

Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni ujenzi wa hospitali za mikoa katika mikoa minne iliyobaki, ujenzi wa hospitali kubwa na ya kisasa ya Binguni pamoja na kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.
Aidha, Mhe. Hemed ameuagiza uongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha kipaumbele cha ajira kinatolewa kwa vijana wazawa wenye sifa na uwezo wa kutoa huduma za afya. Vilevile, amesisitiza kuwepo kwa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) pamoja na wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma za dharura kwa masaa 24, ili kuhakikisha huduma za uhakika za dharura zinapatikana kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali.

Katika hafla hiyo, amewaelekeza wakandarasi na wasimamizi wa mradi kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubalika. Pia amewahimiza wananchi wa Tumbatu kuendelea kutoa ushirikiano na kuilinda miundombinu hiyo ili iweze kuwanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.


Akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025–2030 pamoja na ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, za kuimarisha sekta ya afya na kuboresha ustawi wa jamii.

Amesema kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi zaidi ya 18,366 wa Shehia zote za Tumbatu, kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 30 kwa wakati mmoja na kutoa huduma za afya kwa masaa 24. Kituo hicho kinatarajiwa kutoa huduma za kliniki kwa wagonjwa wa nje (OPD), huduma za mama na mtoto, huduma za dharura na ajali, uchunguzi wa maradhi mbalimbali pamoja na huduma za upasuaji.

Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu unatekelezwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa gharama ya shilingi bilioni 6.4, chini ya Mkandarasi Simba Developer Ltd na unasimamiwa na Idara ya Health Care Engineering and Infrastructure, huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kukifanya Kisiwa cha Tumbatu kuwa wilaya inayojitegemea kutokana na ongezeko la watu. Aidha, amesema kuna haja ya kujengwa soko kubwa na la kisasa ili kufungua fursa za kiuchumi na kukuza biashara kwa wananchi wa kisiwani humo na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ujumla.