Popular services

HAMASA JIMBO LA MKWAJUNI WAFANYA USAFI SOKO LA GAMBA, MSTAHIKI MEYA AHIMIZA USAFI

 

Na Nishan Khamis – Gamba

Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Nyange Kher Ali, amewahimiza vijana pamoja na jamii kwa ujumla kuimarisha usafi katika maeneo ya masoko na sehemu mbalimbali ndani ya wilaya hiyo, ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuifanya Zanzibar kuwa na haiba ya kuvutia kwa usafi.

Meya Nyange ameyasema hayo leo aliposhiriki katika zoezi la usafi katika Soko la Gamba, zoezi lililoandaliwa na vijana wa Hamasa kutoka Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kuwa suala la usafi ni muhimu sana katika kuweka haiba nzuri ya masoko na mazingira kwa ujumla. Aidha, ameongeza kuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo mama katika sekta ya utalii nchini, hivyo kuna kila sababu ya kudumisha usafi sambamba na kulinda amani na utulivu ambao ndio msingi wa maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu wa Hamasa wa Jimbo la Mkwajuni, Kasimu Makame Mwadin, amesema vijana wana nafasi kubwa katika kushiriki shughuli za maendeleo, na kwamba zoezi la usafi ni sehemu muhimu ya uwajibikaji na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Mwinyi katika kuiletea maendeleo Zanzibar.

Naye Muhammad Ibrahim Mussa, mfanyabiashara katika Soko la Gamba, amesema amefurahishwa na jitihada za vijana wa kundi hilo pamoja na ushiriki wa Mstahiki Meya katika kufanya usafi. Amesema kitendo hicho ni cha kupongezwa na amewataka vijana kuendeleza utamaduni huo ili kuboresha mandhari ya masoko na mazingira mbalimbali katika wilaya hiyo.