Na, Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, amehimiza watendaji wa serikali pamoja na wadau mbalimbali kumuunga mkono kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuendeleza maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Gallos ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini “A”.
Amesema kuwa ushirikiano wa pamoja, pamoja na kudumisha amani na utulivu, ni misingi muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo, hivyo amewataka watendaji wa mkoa huo kufanya kazi kwa mshikamano, uadilifu na uwajibikaji.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, amesema anashukuru kuacha mkoa huo ukiwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi chote cha uongozi wake.
Mhe. Mattar amesema mafanikio yaliyopatikana yametokana na umoja na ushirikiano alioupata kutoka kwa watendaji wa serikali na wananchi, na kuwaomba kuendelea kumpa ushirikiano wa dhati Mkuu wa Mkoa mpya kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Aidha, ametoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada kubwa za kimaendeleo anazozitekeleza mkoani humo na Zanzibar kwa ujumla, huku akiwataka watendaji wa serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya viongozi na watendaji waliohudhuria hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Rashid Simai Msaraka, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa mpya ushirikiano wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yake kwa maslahi ya wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.


