Popular services

CCM MKWAJUNI WASOMA DUA MAALUM KULIOMBEA TAIFA, AYOUB AHIMIZA AMANI NA UTULIVU.

 

Na Nishan Khamis, Mkwajuni
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kimefanya dua maalum ya kuliombea taifa kwa kushirikiana na majimbo yote ya wilaya hiyo kufuatia ushindi wa kishindo uliopatikana katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Dua hiyo iliyoandaliwa na viongozi wa jimbo hilo kwa kushirikiana na Kamati ya Siasa, imelenga kushukuru pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuilinda nchi ili amani, utulivu na mshikamano viendelee kudumu kwa misingi ya kuimarisha maendeleo ya taifa.

Katika dua hiyo, waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla wametakiwa kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini ili waweze kunufaika kikamilifu na maendeleo yanayoendelea kusimamiwa na viongozi wa serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika dua hiyo iliyofanyika Msikiti wa Kidombo, Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema kuwa amani ni miongoni mwa tunu kubwa zilizopo nchini na ni wajibu wa kila Mzanzibari kuilinda kwa ajili ya ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe. Ayoub amewasisitiza waumini wa dini hiyo na wananchi kwa ujumla kutokubali kushawishiwa na viongozi au watu wenye nia mbaya ya kuvuruga amani, akieleza kuwa amani ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo endelevu. Aidha, amewataka viongozi wa dini, wanasiasa na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana katika kuhubiri, kutunza amani na kuwaombea dua viongozi wa nchi, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ili waendelee kuiongoza nchi kwa maendeleo zaidi.

Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Kidombo, Mussa Haji Makame, amesema kuwa suala la amani na utulivu limesisitizwa sana katika Uislamu kutokana na umuhimu wake, hivyo jamii ina wajibu wa kuhakikisha tunu hiyo inalindwa na kupewa kipaumbele katika khutba, majukwaa ya kijamii na nyumba zote za ibada.

Aidha, ametoa pongezi kwa viongozi wa CCM Jimbo la Mkwajuni kwa kuandaa dua hiyo muhimu, akiwataka kuendeleza utamaduni huo unaoendana na misingi ya dini, mila na silka za Kiislamu.

Nao wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria katika dua hiyo wamesema wamefurahishwa na hatua hiyo, wakieleza kuwa ni mfano mzuri wa kuenzi mila na silka za Kiislamu badala ya kuiga tamaduni za kigeni zisizoendana na maadili ya jamii.