Popular services

WAZIRI SHAABAN,AFIKISHA SALAAM ZA RAIS DKT . MWINYI KASKAZINI UNGUJA, ASISITIZA KUDUMISHA USAFI.

 Na Nishan Khamis, Zanzibar

Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Mheshimiwa Shaaban Ali Othman, amewasisitiza wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo ili kuimarisha na kupeleka mbele maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Shaaban ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa wilaya pamoja na wananchi, wakati akiwa mgeni rasmi katika zoezi la usafi lililofanyika Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anawasalimia wananchi wa mkoa huo na amewasisitiza kuendelea kudumisha amani na utulivu, kwani ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Aidha amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja ni miongoni mwa mikoa yenye bahati ya kuwa na rasilimali nyingi za kimaendeleo, hivyo ni wajibu wa wananchi na viongozi kuilinda na kuitunza tunu hiyo ili kuongeza kasi ya maendeleo chanya na kuimarisha miundombinu bora ya maendeleo.

Vilevile, amewasisitiza viongozi na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha usafi na kuwa na ratiba za mara kwa mara za kufanya usafi katika maeneo ya bahari pamoja na mazingira yote kwa ujumla, ili kuifanya wilaya hiyo kuwa na haiba nzuri na kuvutia.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa la Wilaya hiyo, Nyange Kher Ali, amemhakikishia mgeni rasmi kuwa baraza hilo litaendelea kusimamia ipasavyo suala la usafi, ikiwa ni kipaumbele cha Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa lengo la kuiweka Zanzibar katika hali ya usafi na haiba ya kuvutia.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Kaskazini A ni miongoni mwa maeneo yanayozungukwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, hivyo kudumisha usafi ni jambo la msingi katika kuvutia watalii, kuongeza pato la taifa pamoja na kujikinga na magonjwa ya milipuko.


Nao baadhi ya washiriki wa zoezi hilo wamesema wamezipokea salamu za Mheshimiwa Rais na kuahidi kuendelea kudumisha amani, utulivu na usafi kwa misingi ya maendeleo ya wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.

Aidha, zoezi hilo lilijumuisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Mstahiki Meya, Mkurugenzi, vyombo vya ulinzi na usalama, watendaji mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Baraza la Manispaa, masheha pamoja na wananchi mbalimbali.