Na Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Jumatatu, 08/09/205.
Mkurugenzi wa Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Mbarouk Maalum Mohammed, amewataka wananchi kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendeleza matumizi ya kilimo hai kwa ajili ya kutunza ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo nchini.
Ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa vikundi vya wakulima wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Walimu Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A.
Amesema miongoni mwa njia bora za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo ni janga la dunia kwa sasa ni jamii kuepuka ukataji miti ovyo na uchomaji wa misitu, na badala yake kujikita katika kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti mingi ili kuleta uwiano wa ikolojia.
Aidha, amewahimiza wakulima wa vikundi kutumia mbinu za kilimo hai kwa kuwa zinasaidia kuhifadhi ardhi kwa muda mrefu, kuongeza ubora wa mazao na kulinda afya za watumiaji nchini.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Arafa Hamad Bakar amesema kilimo hai kina umuhimu mkubwa katika kuongeza uzalishaji, kuboresha rutuba ya ardhi na kuisaidia jamii kujikwamua kiuchumi kutokana na tija inayotokana na mfumo huo wa kilimo.
Amewashauri wakulima hao kutumia mbolea za asili,viatilifu vya asili,kupanda mazao mseto na kuhifadhi na kuongeza rutuba ya udongo kwa maslahi mapana ya kutunza ardhi kwa muda mrefu na kuzalisha mazoa yaliyo bora zaidi.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanashukuru kwa elimu waliyoipata kwani itawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo, ingawa wamesema bado wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa elimu, mikopo na upatikanaji wa maji.
Jumla ya vikundi ishirini vya wakulima vimeshiriki mafunzo hayo, ambayo yameandaliwa na Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini A (JUVIEKA) kwa kushirikiana na Shirika la ActionAid Zanzibar, kwa lengo la kuchochea maendeleo nchini.

