Popular services

JAMII YAHIMIZWA KUHUDHURIA VIKAO KUCHOCHEA MAENDELEO YA SHEHIA

 

Na, Nishan Khamis – Mkokotoni.
Jamii imetakiwa kuwa na utamaduni wa kuhudhuria vikao vya kijamii ili kupanga mikakati ya kimaendeleo, kuibua changamoto zinazowakabili na kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza maendeleo ya shehia na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jana na Afisa Utumishi wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Abdalla Juma Abdalla, kwa niaba ya Mkurugenzi wa baraza hilo, wakati akizungumza na wananchi wa Shehia ya Mkokotoni katika ufunguzi wa kongamano la kijamii lililofanyika kwenye uwanja wa mpira Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Abdalla alisema kuhudhuria vikao vya jamii ni muhimu kwa kuwa kunatoa fursa ya kuibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja kwa maslahi ya maendeleo ya shehia na taifa.
Ameisisitiza jamii kuendeleza utamaduni huo na kushirikiana na viongozi wa ngazi zote katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi, sambamba na kudumisha amani na utulivu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini A (JUVIEKA), Mbarouk Maalum Mohammed, amesema kongamano hilo limetokana na mradi wa Raia Makani unaolenga kuwawezesha wananchi kutambua, kufuatilia na kuchambua bajeti za maendeleo ili kubaini mapungufu na kuimarisha uwajibikaji kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.

Amesema mradi huo unaofadhiliwa na European Union na kutekelezwa Tanzania, ni fursa kwa wananchi wa Zanzibar kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo, kwani maendeleo huanzia ngazi ya chini na si kusubiri viongozi wa juu.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kongamano hilo, akiwemo Mwanakombo Ali Sheha na Mbarouk Omar Zubeir, wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua umuhimu wa kufuatilia shughuli za maendeleo kwa ajili ya kuibua changamoto katika jamii. Wameeleza kuwa kijiji cha Mkokotoni kinakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama, na kupitia mradi huo wanaamini utasaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto hiyo na nyingine katika shehia yao.