Popular services

ZNZ YAPOKEA TANI 25 ZA SADAKA YA NYAMA KUTOKA SAUDI ARABIA


NA FAUZIA MUSSA 

Zanzibar. 

MKURUGENZI wa Mirathi, Zaka na Misaada, Haji Mussa Khatib amesema Serikali itaendelela kushirikiana na wadau wanaotoa misaada ili kuhakikisha  wananchi wake wanapata mahitaji muhimu  kupitia nyanja mbalimbali.

Ameyasema hayo  kwa niaba  ya Katibu Mtendaji wa  Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar wakati wa makabidhiano ya sadaka ya nyama iliyotolewa na Kamisheni ya Kifalme ya Makka na matokeo matakatifu kupitia mradi wa Ufalme wa Saudi Arabia wa kutumia nyama ya Hijja (Adahi), hafla iliyofanyika ukumbi wa kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana Mazizini.

Alisema Sadaka hiyo imekusudiwa wananchi wa Zanzibar na kuwa itamfikia kila mlengwa kwa utaratibu maalum Unguja na Pemba.

“Ugavi wa nyama hii utafanyika katika Wilaya zote za Zanzibar kwa makundi maalum na mtu mmoja mmoja hasa wale waliyoko vijijini ambao uzowefu unaonesha kuwa sio rahisi kufikiwa mara kwa mara.” Alifafanua 

Alifahamisha kuwa nchi mbili hizo zimekuwa na undugu wa muda mrefu kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo ya misaada na taaluma na kuwa kitendo hicho kitaendeleza mahusiano hayo.


Alisema wakati wa kugawa nyama hiyo kamisheni ya wakfu itazingatia hali ya umasikini na idadi ya watu kulingana na matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 na kutowa kipaumbele kwa wenye mazingira magumu na wasiyojiweza.

Naye Mwakilishi wa Ubalozi wa Saudia Arabia Nchini Tanzania, Fahad Alsharar alisema takriban kondoo elfu tano walichinjwa na kupatikana tani 25 za nyama iliyogharimu dola laki 9 na sitini elfu na bil2.4 na kukabidhiwa  kamisheni ya wakfu na mali ya amana ili  nao wawapatie wanaostahiki.

“Nyama hii imetokana na mradi wa Ufalme wa Saudi Arabia wa kutumia nyama ya Hijja (Adahi), ambapo shehena ya nyama iliyogandishwa katoni 1,710, vifurushi 17,100 vya mtu mmoja mmoja, vilisafirishwa katika makontena matatu ya friji na kufika katika Bandari ya Zanzibar na kukabidhiwa Kamisheni ya wakfu  kwa kuwagaia walengwa wanaostahili.” Alifahamisha mwakilishi huyo

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa bodi ya kamisheni ya wakfu na mali ya amana, Issa Haji Zidi alisema ni vyema kuyaendeleza  mahusiano hayo ambayo huleta tija kwa wananchi wa Zanzibar.

 Zidi alitumia fursa hiyo  kuushukuru ubalozi wa Saudia Arabia Nchini Tanzania kwa kutokana na wanovvyielekeza misaada hiyo ndani ya Zanzibar pasi na hiyana na kwaomba kuongeza misaada zaidi kutokana na kuwa nchi ya Zanzibar inaendelea kukuwa, hivyo  kuongezeka idadi ya wenye uhitaji.

Mkaguguzi wa Chakula ZFDA, Amina  Rashid, alithibitisha kuwa sampuli za nyama hiyo zimeshachukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa usalama kabla ya kugawiwa kwa walengwa ili kubaini usalama wa mtumiaji. 

Idara ya Habari Maelezo Zanzibar