Popular services

WAVUVI WASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA ZASFICU KWA MAENDELEO BORA YA WAVUVI NCHINI.


Na,Nishan khamis
Zanzibar.

Wavuvi wadogo wadogo na jamii kwa ujumla wametakiwa kushirikiana na chama cha wavuvi wadogo wadogo Zanzibar(ZASFICU) ili kujenga umoja na ushirikiano utakao pelekea kutumia fursa mbali mbali zilizopo baharini kwa maendeleo bora ya wavuvi wadogo wadogo na taifa kwa ujumla.

Haya ameyasema mwenyekiti wa vyama vya Muungano wa vyama vya ushirika Zanzibar(CUZA) leo ndugu Suleiman Ame Mbarouk alipokuwa akizungumza na viongozi wa ZASFICU, wataalam wa tafiti mbali mbali, maafisa uvivu na wanavikundi vya uvuvi nchini katika mkutano mkuu mwaka  wa chama cha ZASFICU uliofanyika katika ukumbi wa mikutano kituo cha walimu Mkwajuni wilaya ya kaskazini A Unguja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mwenyekiti Suleimana amesema bahari ina fursa nyingi za kujikwamua kiuchumi kwa jamiii kwani ajira nyingi nchini zinatokana na uchumi wa buluu hivyo ikiwa wavuvi wakishirikiana kwa pamoja na ZASFICU ni jambo la msingi katika kuisadia serikali kuendelea kutekeleza azma yake katika kuimarisha maisha bora ya wavuvi kama sera ya uchumi wa buluu na marais wote nchini azma zao katika kuwainua kiuchumi wajasiriamali wadogo wadogo nchini.

Hivyo ametoa wito kwa vijana kukimbilia fursa hizo pamoja na ZASFICU kuongeza wanachama wapya zaidi ili kuwasaidia zaidi wavuvi wadogo wadogo kuwa na maisha bora katika nyanza zote za shughuli za baharini.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika mkutano huo mwenyekiti wa ZASFICU ndugu Omar Moh'd Ali amesema lengo la chama hicho ni chombo cha kuwasemea wavuvi wadogo wadogo nchini katika kuhakikisha kuwa wanakuwa na maisha bora, safi na salama ,waweze kuwa na sauti moja katika kusimamia utetezi wa sera na sheria kwa wavuvi ili kuisaidia serikali katika kuongeza   ajira nyingi nchini.

Rahma Khatib akisoma risala katika hafla hiyo amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2023 na kupata usajili rasmi mwaka 2023 ambapo mpaka kufikia leo wanajumla ya wanachma wa vikundi 57 na vikundi vingine vikiendelea na taratibu za kujiunga za ZASFICU ili kuendelea kuongeza nguvu zaidi katika kuimarisha maisha bora ya wavuvi ikiwa ni lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt Husein Ali Mwinyi na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan katika mikakati ya kuwajengea mazingira bora ya kuwainua kiuchumi zaidi wavuvi nchini.

Pia alibainisha uwepo wa ofisi ndogo kwa upande wa Unguja na kukosekana ofisi pemba ni changamoto kubwa kwao inayokwamisha utekelezaji wa ufanisi wa shughuli zao.

Nae Fatma Abdalla Jaha akitoa taarifa za matumizi ya mapato za ZASFICU mwaka 2023-2024 amesema chama hicho kimekuwa na vyanzo vya mapato katika kiingilio,ada,michango na hisa ambapo ndani ya miaka hiyo wamekusanya shilingi milioni 9 laki 1 na 79 elfu na kiasi cha matumizi katika mwaka huo ni shilingi milioni 4 laki 8 na 91 elfu.

Kwa upande wake afisa uvivu kutoka wilaya ndogo Tumbatu Amour Sheha Khamis amewashauri wavuvi kuanzisha vikundi rasmi ambavyo vitawasaidia kupata mikopo kwa haraka ili kuimarisha shughuli zao kuliko kuomba mikopo hiyo kwa mtu binasfi ni jambo ambalo changamoto katika upatikanaji wa mikopo kwa wavuvi.

Nao baadhi ya wavuvi waliohudhuria mkutano huo wamesema wanashukuru serikali zote kwa jitihada zao za kuwainua kiuchumi jambo ambalo linawapa moyo kutoka katika uvivu mdogo mdogo na kwenda uvivu mkubwa ambapo wameiomba ZASFICU kuendelea kuwasema changamoto zao hasa za mikopo na sera na sheria ili kuwainua ziadi wavuvi wadogo wadogo nchini.