NA MWANDISHI MAALUM.
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu ili kufikia azma ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Hatua hiyo inakwenda sanjari na kusomesha watoto wa Kitanzania na kuzalisha watalaamu wenye ujuzi watakaokabili ushindani katika soko la ajira.
Dk. Samia alieleza hayo baada ya kufungua skuli ya sekondari ya Balozi Seif Ali Idi iliyopo Bubwini Misufini, wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 61 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Alisema mtu anaweza kuwa msomi lakini alichokisoma hakiwezi kumsaidia wala taifa, lakini akiwa mtalamu wa eneo fulani basi utaalamu huo akiutumia utamsaidia na taifa kwa ujumla.
Alibainisha kuwa zipo ajira nyingi ambazo vijana wa kizanzibari wanazikosa kutokana na kukosa ujuzi na kuchukuliwa na vijana kutoka Tanzania bara.
Alisema Tanzania imezindua mkakati wa uchumi wa kidijitali ambao umejielekeza kufanya kazi na sekta binafsi kwa kualika wawekezaji hivyo wameaua kujaza kompyuta maskulini ili kutayarisha vijana waweze kuajirika kwani hivi sasa mambo yote ni kidojitali.
Hivyo, aliwasisitiza wazazi na walezi kutimiza wajibu katika kuhimiza watoto kusoma kwa bidii kwani serikali inafanya jitihada kuweka mazingira mazuri ili waweze kusoma kwa bidii na kuwapa fursa watoto kutumia matunda hayo
Akizungumzia malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Dk. Samia alisema miaka 61 imeifikisha nchi katika pahala mazuri na nchi inaendelea hatua kwa hatua.
Alisema wazee waliweka misingi mizuri na kuendana na amri ya dini na jambo la kwanza ni kusoma na walioleta mapinduzi walisema elimu bure kwa watoto wote.
Alibainisha kuwa baada ya wao kupewa fursa na kujua umuhimu wa elimu nao awamu kwa awamu wamekuwa wakiboresha sekta hiyo ili kuona watoto wanasoma katika mazingira mazuri.
Akizungumzia kusoma kwa kutumia mtandao alisema hapo ndipo Mapinduzi yalikuwa yanapelekea kwani Mapinduzi ni maendeleo hatua kwa hatua na kusisitiza kwamba mapinduzi ya kutafuta uhuru yamemalizika na hivi sasa ni maendeleo na kulinda uhuru wao ambao ndio mapinduzi yao kwa sasa.
Dk. Samia alisema miaka ya nyuma walipokuwa walifanya mitihani ya kidato cha nne Zanzibar ilikuwa chini kimatokeo kutokana na wanafunzi kutofundishwa kwa vitendo kutokana na kukosa maabada katika skuli, lakini hivi sasa wameweka vifaa vya kisasa ikiwemo kompyuta.
Aliwataka walimu kuboresha ujuzi wao kupitia kompyuta hizo ili kuwa mwalimu mzuri na bora na vyumba hivyo vya kujifunza kivitendo vitatumika vizuri.
Dk. Samia alisema kabla ya Mapinduzi Zanzibar walikuwa na skuli 62 ikiwemo za sekondari tano na maandalizi moja lakini hivi sasa kuna skuli 1,308 za msingi, sekondari na michipuo na vyuo vikuu.
Alisema hayo yote ni kuwatayarisha watoto kuwa viongozi wa baadae hayo ndio maendeleo na matunda ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Dk. Samia alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa uangozi thabit na maono ya maendeleo anayoyafanya ndani ya nchi.
Sambamba na hayo, Dk. Samia aliwapongeza wananchi wa Kaskazini kwa kushirikiana na serikali hasa wale ambao wanatoa maeneo yao kwa ajili ya miradi kujiletea maendeleo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alisema alisema serikali ya SMT na SMZ zimewekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu, maslahi ya walimu na vifaa na kuweka mifumo ya Tehama ili kuona elimu inatolewa kisasa zaidi.
Alibainisha kuwa hadi sasa serikali imeshajenga skuli za ghorofa 35 na ghorofa 28 zipo katika hatua za mwisho za ujenzi na kukarabati skuli zote chakavu ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kwa mradi wa ujenzi wa skuli hiyo, Katibu wa Wizara hiyo, Khamis Abdalla Said, alisema ujenzi wa skuli hiyo ulianza rasmi mwezi Septemba mwaka 2023 na kukamilika Disemba 2024 ambapo imejengwa na kampuni ya Simba Davelelopa chini ya mshauri elekezi AE & Q Consulting Limited ambapo thamani ya skuli hiyo ni shilingi bilioni 6.1.
Alisema skuli hiyo ya ghorofa tatu ina madarasa 40, vyoo 29, ofisi ya Mwalimu Mkuu na Walimu wasaidizi, ofisi za walimu, maabara mbili za kisasa, chumba cha Tehama, chumba cha kusalia na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,800 kwa wakati mmoja kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.


