Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Mattar Zahor Masoud, amesisitiza umuhimu wa mshikamano, utunzaji wa amani, na malezi ya maadili kwa watoto, sambamba na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya harambee ya uchangiaji wa Redio ya Anour FM iliyofanyika leo katika Msikiti wa Ijtima, Kidoti, Wilaya ya Kaskazini A – Unguja, Mheshimiwa Mattar alisema kuwa lengo la hafla hiyo ni kuimarisha ushirikiano miongoni mwa waumini wa Kiislamu katika kuendeleza dini kupitia redio hiyo.
Katika hotuba yake, RC Mattar alieleza kuwa Uislamu unahimiza mshikamano na ushirikiano kwa misingi ya kuendeleza maendeleo ya dini. Alitoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika malezi ya watoto na kupambana na vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinasababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Aidha, alitoa salamu kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa waumini hao, akieleza kuwa Rais anatambua na kuthamini tukio hilo, na yupo pamoja nao kwa moyo mmoja. Aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, na kuwahakikishia kuwa hali ya utulivu itaendelea kudumishwa katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Redio ya Anour FM, Ali Mkubwa Zubeir, aliwashukuru waumini, mgeni rasmi, serikali, na wahisani mbalimbali kwa mchango wao wa dhati katika kusaidia kuendeleza redio hiyo.
Alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, kituo hicho kimepitia changamoto za ukosefu wa ufadhili, lakini kwa msaada wa wadau wameendelea kulingania dini na kuelimisha umma juu ya masuala mbalimbali ya kijamii na kidini kwa manufaa ya duniani na akhera.
Aliweka wazi kuwa redio hiyo itaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, na kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza amani, utulivu na kupinga vitendo vyote viovu katika jamii, kwa kuzingatia kaulimbiu yao ni muangaza kwa umma.
Waumini waliohudhuria hafla hiyo walisema kuwa ni jukumu la Waislamu wenyewe kuendeleza dini yao, hivyo kushiriki katika harambee kama hiyo ni wajibu kwa maslahi ya sasa na baadae. Walisema kuwa Uislamu ni dini ya amani na upendo, na wanapaswa kuendeleza utulivu uliopo nchini.
Katika harambee hiyo, jumla ya shilingi milioni 17, laki 4 na elfu 95 zilichangishwa, ambapo Mkuu wa Mkoa huyo alitoa mchango wa shilingi milioni 5 taslimu na kuhamasisha waumini wengine kuendelea kuchangia kwa moyo mmoja.


