Nishan Khamis, Kaskazini Unguja.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Bi Lucy John Mpembo, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Nungwi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo ameshiriki katika Mkutano Mkuu Maalum wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwachagua wagombea wa nafasi za Ubunge na Uwakilishi kupitia UWT kwa mkoa huo, na umehudhuriwa na wajumbe kutoka wilaya zote za mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza katika mkutano huo, Bi Mpembo amepongeza uongozi wa UWT kwa kuratibu vyema mchakato huo muhimu wa kidemokrasia ndani ya chama, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wanawake na ushiriki wao katika uongozi wa kisiasa.
“Tuna jukumu kubwa kama wanawake kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika uongozi, ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu,” alisema Bi Mpembo.
Mkutano huo ni sehemu ya mchakato wa ndani ya CCM kupitia jumuiya zake, ukilenga kuwapata wagombea wenye sifa na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji.
