Popular services

ASHA SULEIMAN NIYA YA KUGOMBEA NAFASI YA UWAKILISHI PEMBA KUPITIA CHAMA CHA ADA-TADEA, AMWAGA MAUA KWA DKT. SAMIA NA DKT. MWINYI


Na,Nishan khamis- kaskazini Unguja.

Asha Suleiman, mwanamke  mpenda maendeleo, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya Uwakilishi kisiwani Pemba kupitia Chama cha ADA-TADEA. Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Asha amesema dhamira yake kuu ni kuwahudumia wananchi kwa uadilifu, huku akilenga zaidi katika kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Asha amesema kuwa ameamua kuchukua hatua ya kugombea baada ya kutambua kuwa uongozi ni fursa ya kipekee kwa mwanamke kuleta mabadiliko chanya katika jamii. "Nimekidhi vigezo vya kiuongozi na naamini nina sifa za kutosha kuchangia maendeleo ya watu wetu. Nimejifunza, nimelelewa na nimejiandaa kuhudumu kwa moyo wa dhati," amesema.

Aidha, Asha amewaomba wanawake wote, vijana na jamii kwa ujumla kumpa ushirikiano katika safari hii ya kisiasa, akisisitiza kuwa mafanikio ya mwanamke mmoja ni chachu ya mafanikio ya jamii nzima. Amehamasisha wanawake wengine wasikimbie siasa bali wakimbilie fursa, wajitokeze na kushiriki katika uongozi kwa ujasiri na uthubutu.

Katika hotuba yake, Asha Suleiman amewapongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna wanavyowainua wanawake katika nafasi za uongozi, jambo linaloonyesha dhamira yao ya kweli ya usawa wa kijinsia.

Mwisho, Asha Suleiman amesisitiza kuwa iwapo atapewa nafasi, ataendelea kuwa sauti ya wanyonge, mtetezi wa haki za wanawake na mfano wa kuigwa kwa kizazi kijacho cha viongozi wanawake nchini.