Popular services

RC MATTAR: TUMEJIPANGA KUTOKOMEZA VITENDO VIOVU NA KUIMARISHA UFAULU WA WANAFUNZI KASKAZINI UNGUJA


Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Mattar Zahor Masoud, amesema kuwa Serikali ya Mkoa huo imeandaa mikakati madhubuti ya kupambana na vitendo viovu kama vile wizi, matumizi ya dawa za kulevya, na biashara ya ukahaba ambavyo vinahatarisha ustawi wa jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Mkoa wa kaskazini Unguja, katika kikao chake cha kila mwezi, RC Mattar alieleza kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wilaya pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama imejipanga kwa pamoja kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kabisa kwa lengo la kudumisha amani na usalama wa wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo husika katika kukabiliana na uhalifu, huku akisisitiza umuhimu wa kuachana na muhali na kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo.

Mhe. Mattar pia alieleza kuwa Serikali ina mipango mizuri ya maendeleo ya mkoa, na hivyo ni vyema wananchi wakaungana kwa pamoja katika kuyatekeleza na kuyaendeleza kwa manufaa ya jamii. Pia aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wa elimu, RC Mattar alisema kuwa hajaridhishwa kwa kiasi kidogo na matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2024, na kwamba Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na walimu na kamati za skuli imeanza kuchukua hatua za kuondoa kabisa matokeo ya division zero. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wazazi katika kuwahimiza watoto wao kujifunza kwa bidii ili kuinua kiwango cha ufaulu.

Baadhi ya wananchi wa mkoa huo waliongea kwa nyakati tofauti, waliiomba Serikali kuendelea na oparesheni za mara kwa mara za kukabiliana na uhalifu, hususan uuzaji wa dawa za kulevya, wizi wa mazao na mifugo, ili kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.