Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja
Uchaguzi wa nafasi za udiwani kupitia viti maalum vya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja kwa mwaka 2025 umekamilika kwa amani na utulivu, ambapo jumla ya wagombea 15 walishiriki katika kuwania nafasi hizo.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Farid Ali Mohammed, alitangaza kuwa jumla ya kura zilizosajiliwa ni 796, kura zilizopigwa 727, kura halali 692 na kura zilizoharibika ni 35.
Wagombea waliopata ushindi ni Faida Salmin (kura 358), Subira Ali Juma (329), Maimuna Kasimu (327), Hawa Ubwa Mchezo (312), na Kombo Haji Fum (282); ambao ndio waliongoza kwa kura nyingi kati ya wagombea wote.
Katibu wa UWT wa wilaya hiyo, Mtenge Makame Faki, alitoa shukrani kwa wajumbe wote walioshiriki na kusimamia uchaguzi huo, akieleza kuwa mchakato mzima umefanyika kwa amani na mshikamano mkubwa. Aidha, alitaja ukosefu wa ukumbi wa mikutano kama changamoto iliyojitokeza na kuomba chama kuhakikisha kuwa ujenzi wa ofisi ya wilaya unakamilika haraka.
Alisisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi bado unaendelea kwa hatua nyingine za kisiasa na kiutendaji ndani ya chama, hivyo wanachama wanapaswa kuendelea kushiriki kwa umoja na mshikamano.
Washindi wa uchaguzi huo walitoa pongezi kwa wajumbe na wasimamizi wa uchaguzi pamoja na uongozi wa UWT na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Waliahidi kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na kwa maslahi ya wanawake, chama na taifa kwa ujumla.
Wajumbe walioshiriki uchaguzi huo walieleza kuridhishwa kwao na uendeshaji wa uchaguzi huo kwa haki, uwazi na utulivu. Walihimiza viongozi waliochaguliwa kutumia nafasi walizopewa katika kushughulikia changamoto mbalimbali na kuendeleza ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla.
