Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Afisa Ramadhan Khamis Makame, ameitaka jamii ya mkoa huo kushirikiana kwa karibu na idara yake katika kudhibiti uhamiaji haramu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake iliyopo Kivunge, Wilaya ya Kaskazini A, Kamishna Ramadhan amesema kampeni ya “Mjue Jirani Yako” inayoendelea mkoani humo inalenga kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa za wageni wasiowafahamu katika maeneo yao, ili kusaidia juhudi za kudhibiti uhamiaji haramu.
Amesisitiza kuwa elimu hii ina umuhimu mkubwa katika kulinda usalama wa jamii na taifa kwa ujumla, akihimiza taarifa zote ziwafikie masheha au ofisi za idara ya uhamiaji kwa haraka na usahihi.
Aidha, katika mwendelezo wa kampeni hiyo, mafunzo maalum yamefanyika katika Skuli ya Mkokotoni kwa kushirikisha walimu na wanafunzi, ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa. Mada hizo zimegusia huduma za ndani zinazotolewa na idara hiyo, ikiwemo masuala ya uraia, taratibu za upatikanaji wa vibali, masharti ya ukaazi kwa wageni, pamoja na sifa zinazomtambulisha mgeni halali anayepaswa kuwepo nchini.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mrakibu wa Uhamiaji Amina Ali Khamis alisema kuwa lengo kuu ni kuwaelimisha washiriki namna ya kutambua wageni waliopo kihalali au kiharamu kwa lengo la kuimarisha usalama wa nchi, kuongeza mapato ya taifa, pamoja na kuelewa haki na usawa wa kijamii.
Aliongeza kuwa uhamiaji haramu una madhara makubwa, yakiwemo mmomonyoko wa maadili, kushamiri kwa vitendo vya kihalifu, upotevu wa mapato ya taifa, na kuathiri taswira ya usalama wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wao, walimu Mbaraka Nyona na Khadija Machano Khamis walisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ambacho mara nyingi huambatana na ongezeko la watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu. Waliahidi kuwa mabalozi wa kushirikiana na idara hiyo katika kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa.


