Popular services

NAPAC NA UNDP WAZINDUA KAMPENI YA ELIMU YA KISHERIA SHEHIA 44 ZA WILAYA KASK "A".


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imezindua kampeni ya utoaji wa elimu ya kisheria kwa jamii kupitia mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa kwa washiriki kutoka shehia 44 za wilaya hiyo. Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa LEAP II (Legal Empowerment and Access to Justice Program) unaofadhiliwa na UNDP.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa TC Mkwajuni, Mkurugenzi wa NAPAC, Asia Fadhil Makame, amesema bado jamii nyingi hazina uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kisheria, jambo linalowafanya washindwe kudai haki zao. Kupitia mafunzo haya, jamii itapata uelewa wa njia sahihi za kufikia haki zao hasa wanawake na makundi maalumu.

Asia aliipongeza UNDP kwa kuendelea kufadhili miradi ya kuwawezesha wananchi kielimu na kisheria, huku akiwasihi wananchi kushirikiana na NAPAC ambayo hutoa huduma za kisheria bila malipo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuzitambua na kuzifikia haki zao za msingi.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, alitoa pongezi kwa UNDP na NAPAC kwa mchango wao mkubwa wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi. Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wananchi kupata haki zao na hivyo aliwataka washiriki kuwa mabalozi wa elimu hiyo katika jamii zao.



Aidha, alitoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji, pamoja na kulinda amani na kuchagua viongozi sahihi kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Wakufunzi wa mafunzo hayo, Bi. Hadia Ali Makame na Salma Ibrahim Juma kutoka NAPAC, waliwasilisha mada mbalimbali ikiwemo: udhalilishaji, utamaduni wa muundo wa mahakama, utambuzi wa haki za binadamu, na sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2006 Zanzibar.

Walisisitiza kuwa ni muhimu jamii itambue kuwa watu wenye ulemavu wana haki sawa kama wengine na vitendo vya udhalilishaji dhidi yao ni kosa la jinai kisheria.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Asia Othman, alieleza furaha yake kwa kushiriki katika mafunzo hayo, akisema yamekuwa hazina muhimu kwake na ameahidi kuwa balozi wa elimu hiyo katika jamii yake kwa maendeleo ya pamoja.