Popular services

BI ULAYA, KATIBU WA WATU WENYE ULEMAVU NA MWANAMKE SHUJAA, ALIYENYAKUA TUZO YA MFANYAKAZI BORA AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO


Na,Nishan khamis -kaskazini Unguja.

Katika tukio la kipekee lililofanyika hivi karibuni katika Ofisi ya Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Bi Ulaya Khamis Juma ametunukiwa tuzo ya Mfanyakazi Bora, hatua inayodhihirisha uwezo, juhudi, na kujitolea kwa watu wenye ulemavu katika nyanja za uongozi na huduma kwa jamii.

Bi Ulaya ni Katibu wa Watu Wenye Ulemavu katika Wilaya ya Kaskazini A Unguja pamoja na kuwa Mjumbe hai wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya hiyo (NAPAC). Ameendelea kuwa sauti ya matumaini kwa watu wenye ulemavu, akitetea haki, fursa sawa, na ushiriki wa watu wenye mahitaji maalum katika maendeleo ya jamii.

Kupitia kazi yake ndani ya jamii, Bi Ulaya ameonesha uongozi wa mfano kwa kutumia ulemavu wake kama daraja la kuunganisha watu badala ya kuwa kikwazo. Uwepo wake katika nafasi za maamuzi umekuwa ni chachu ya mabadiliko chanya, hasa katika maeneo ya usawa wa kijinsia, ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu, na upatikanaji wa huduma za msingi.

Moja ya mafanikio yake makubwa yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu na wafanyakazi wenzake ambapo ametoa wito kwa wanawake kufanya kazi kwa kujitolea bidiii,nidhamu kwa hali na mali pamoja na kuzikimbilia fursa za uongozi katika nyanza zote nchini.

 Wenzake wanamsifu kwa kuwa mchapakazi, mwepesi wa kushirikiana, na mwenye moyo wa kujenga timu. Wanamwelezea kama mtu anayeheshimu mawazo ya wengine, anayehamasisha mshikamano kazini, na ambaye yuko tayari kuwasaidia wengine katika majukumu ya kila siku. Uwepo wake umeimarisha si tu uwajibikaji ndani ya ofisi, bali pia mshikamano wa kiutumishi unaochochea maendeleo ya kweli.


Pia wamempongeza kwa ushindi huo na kueleza kufurahishwa kwao na utendaji wake bora wa kazi pamoja na ushirikiano mkubwa anaoonesha katika kuwahudumia wananchi, hususan watu wenye ulemavu, wanawake na watoto. Wamesema kuwa Bi Ulaya ni mfano wa kuigwa na amekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha kila mtu anapata huduma stahiki bila ubaguzi, hali inayodhihirisha uongozi wenye maono, huruma na uwajibikaji wa kweli.