Popular services

VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UONGOZI HASA KUELEKEA UCHAGUZI 2025.


Na: Nishan Khamis, Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ZAFAYCO, Abdalla Abeid, amewataka vijana wa Kizanzibari kuwa mstari wa mbele katika kuchangamkia nafasi za uongozi nchini, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Amewahimiza vijana kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo ili kuongeza idadi yao katika vyombo vya maamuzi.

Abdalla alitoa wito huo jana katika mjadala uliowakutanisha taasisi za vijana, taasisi za serikali na binafsi, viongozi wa dini, pamoja na wawakilishi wa vijana kutoka Unguja na Pemba. Mjadala huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano Kariakoo, Wilaya ya Mjini, ukilenga nafasi ya vijana katika mchakato wa kidemokrasia kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.

Amesisitiza kuwa lengo ni kujenga maendeleo ya taifa na kuhimiza vijana pamoja na taasisi mbalimbali kuwa mabalozi wa amani na upendo kwa ajili ya maslahi ya kitaifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Muhamed, ameipongeza ZAFAYCO kwa jitihada zake katika kutekeleza kwa vitendo Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2023. Amesema ushiriki wa vijana katika demokrasia ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, na akawahimiza kuripoti vitendo vya rushwa hususan kipindi hiki kuelekea uchaguzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA-Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa, na Mkurugenzi wa PYI, Rashid Mwinyi, wamesema kuwa changamoto kama elimu ndogo ya uraia, kutokuwepo kwa madawati ya jinsia, na mazingira hatarishi ya uchaguzi bado ni kikwazo kwa ushiriki wa vijana katika uongozi pamoja na mchakato wa uchaguzi. 

Wamewasihi vijana kujitokeza kwa nguvu zaidi kuwania nafasi hizo huku wakizitaka mamlaka husika kuzifanyia kazi changamoto zilizopo. Vilevile, wamewahimiza vijana kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kama njia ya kupaza sauti zao na kuleta mabadiliko chanya.

Kwa upande wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Kisheria, Maulid A. Mohamed, amesema kuwa asilimia 80 ya vijana wamejitokeza katika uandikishaji wa wapiga kura, jambo linaloonyesha taswira nzuri ya ushiriki wao katika uchaguzi. Ameeleza kuwa tume hiyo inaongozwa kisheria na mabadiliko mbalimbali yamefanyika kutokana na maoni ya wadau.

Mjadala huo umeandaliwa na taasisi ya ZAFAYCO kwa kushirikiana na taasisi ya konrad adenauer stiftung(KAS) kutoka nchini Ujerumani.