Kiungo Mchezeshaji: No. 8 Nishan Khamis – Nungwi
Taasisi binafsi ya Mama Africa Children Association yenye makao yake Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, leo imekutana na timu za vijana za Kundemba FC na Shaba FC kutoka Nungwi, ambapo imetekeleza ahadi ya kukabidhi vifaa vya michezo ya mpira wa miguu kwa ajili ya timu hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Jamila Kallaghe, amesema kuwa taasisi yao inajihusisha na masuala ya watoto, wanawake, na vijana. Alisema kuwa kutokana na changamoto ya ukosefu wa vifaa kwa vijana hao, taasisi hiyo iliona ni muhimu kutoa msaada huo ili kuwasaidia katika harakati zao za michezo. Alisisitiza kuwa lengo ni kuongeza hamasa kwa vijana na kuunga mkono juhudi za marais wote nchini katika kukuza sekta ya michezo, hasa kwa vijana.
Jamila alisisitiza kuwa vijana wa Nungwi wanapaswa kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuleta maendeleo chanya katika michezo, kwa maslahi yao binafsi, familia zao, na taifa kwa ujumla.
Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bi. Lucy John Mpembo, alisema kuwa michezo ni afya na ajira yenye thamani kubwa duniani leo. Alisisitiza kwa vijana hao kutumia fursa ya vifaa walivyokabidhiwa ili kujitahidi zaidi katika michezo na kufikia malengo yao katika soka. Aliwahimiza kutokuwa na kukata tamaa kutokana na changamoto zinazowakabili, bali wawe na juhudi, nidhamu, na kumtegemea Mungu ili kufanikiwa. Aliahidi kuwa taasisi yao itaendelea kushirikiana nao kwa hali na mali ili kuinua vipaji vya vijana katika mchezo wa soka.
Aidha, Bi. Lucy alisisitiza kuwa michezo ni fursa nzuri ya kuhamasisha amani, ushirikiano, na upendo nchini, na aliwashauri vijana kutokubali kuingizwa kwenye mivutano inayoweza kuvunja amani ya nchi.
Mama Africa Children Association ilikabidhi mipira, jezi, na vifaa vingine vya michezo kwa timu hizo, huku ikiahidi kuendelea kutoa msaada wa vifaa zaidi ili kuwezesha vijana hao kufanya vizuri katika michezo, kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, manahodha wa timu za Kundemba FC na Shaba FC walitoa pongezi za dhati kwa taasisi hiyo na viongozi wote kwa utekelezaji wa ahadi hiyo kwa vitendo. Walisema kuwa vifaa hivyo vitasaidia sana katika masuala yao ya michezo na kuongeza hamasa katika mazoezi, kwa matumaini ya kufika mbali katika soka la ndani na nje ya nchi. Walieleza pia ombi kwa taasisi hiyo kuwa msaada wao hautaishia hapa, na kwamba wataendelea kushirikiana nao katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kimichezo.
Waliomba pia taasisi zingine kuunga mkono juhudi za Mama Africa Children Association katika kusaidia jamii, hasa watoto, wanawake, na vijana katika kijiji cha Nungwi.
.

