Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, amelitaka Baraza la Vijana Wilaya ya Kaskazini A Unguja pamoja na mabaraza ya vijana ngazi ya shehia kuwajibika kikamilifu katika kuimarisha ufanisi wa mabaraza hayo, sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kutunza na kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa leo katika ziara yake maalum ya kukutana na viongozi wa Baraza la Vijana la wilaya hiyo na kamati tendaji yake, pamoja na kutembelea miradi ya uhifadhi wa mazingira katika shehia ya Pale na mradi wa upandaji mikoko katika shehia ya Mto wa Pwani.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Mtendaji amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mpango mkakati wa mwaka 2024–2025 unaolenga kuimarisha mabaraza ya vijana nchini kwa kutengeneza fursa na programu mbalimbali zitakazochochea maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla. Hivyo, amewataka viongozi wa mabaraza hayo kuwa na uwajibikaji wa hali ya juu katika kubuni programu na kushirikiana na taasisi pamoja na wadau mbalimbali ili kuendeleza maendeleo ya vijana nchini.
Katika ziara hiyo kwa nyakati tofauti,katibu ameyapongeza mabaraza ya vijana ya shehia za Pale na Mto wa Pwani kwa juhudi zao katika utunzaji wa mazingira, akisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za viongozi wakuu wa nchi katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amewahimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika majukumu ya kuhifadhi mazingira, huku akiahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizopo katika mabaraza na miradi hiyo ili kuleta maendeleo yenye tija kwa vijana nchini. Pia amewahamasisha vijana kuendeleza amani na mshikamano ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya hiyo, Ndugu Khamis Adamu Mlekwa, amempongeza Katibu Mtendaji na ujumbe alioambatana nao kwa ziara hiyo, huku akiahidi kuyafanyia kazi maagizo na ushauri waliopatiwa kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya kwa mabaraza ya vijana katika ngazi zote za wilaya na shehia.
Naye Katibu wa Baraza hilo, Ndugu Nassor Haji Makame, ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayokabili mabaraza ya vijana ni jiografia ya wilaya hiyo, jambo linaloathiri ushiriki wa vijana. Hata hivyo, ameahidi kuwa wataandaa mikakati madhubuti ya kuongeza wanachama ili kuimarisha nguvu ya pamoja na kuleta maendeleo ya kweli katika mabaraza hayo.
Kwa upande wao, Nali Bakar Foum, Katibu wa Baraza la Vijana Shehia ya Pale, na Mohamed Juma, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mto wa Pwani, wamemshukuru Katibu Mtendaji kwa ziara yake, wakisema kuwa imewapa hamasa na motisha mpya katika kazi zao. Wameeleza pia kuwa changamoto kama ukosefu wa elimu, wizi na uhaba wa fedha bado zinakwamisha juhudi za uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao.




