Popular services

KAMPENI YA MJUE JIRANI YAKO YAZIDI KUTIA MZIZI KUSINI UNGUJA,WANANCHI WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA WAHAMIAJI HARAMU NCHINI.


Na: Nishan Khamis – Kusini Unguja
Aprili 22, 2025

Katika jitihada za kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu nchini, wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wamehimizwa kushirikiana kwa karibu na Idara ya Uhamiaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa za wahamiaji hao.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Tunguu, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji na Naibu Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kusini Unguja, Paul Makonyu Stephen alisema kuwa Idara hiyo imeanzisha kampeni maalum iitwayo "Mjue Jirani Yako", yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kudhibiti vitendo vya uhamiaji haramu.

“Kampeni hii inalenga kupunguza wimbi la wahamiaji haramu nchini, na tunashukuru wananchi wa mkoa huu wameipokea vizuri. Ingawa changamoto bado ipo, lakini kwa mikakati madhubuti, tumepunguza kwa kiasi kikubwa uingiaji wa wahamiaji haramu katika mkoa huu,” alisema Afande Makonyu.

Ameongeza kuwa wageni wote wanaoingia katika mkoa huo wanapaswa kufuata taratibu rasmi za uingiaji nchini, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji na Mwanasheria wa Idara hiyo, Bakar Ali Kombo, akizungumza katika kijiji cha Uroa alisema kuwa wahamiaji haramu huleta athari mbalimbali katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na pia kuchochea vitendo vya kihalifu. Amehimiza wananchi kutoa taarifa kwa Sheha au Idara ya Uhamiaji mara wanapowatilia mashaka wageni katika maeneo yao.

Ameeleza pia kuwa kuna mpango wa kuweka askari wa uhamiaji katika kila shehia ili kusaidia katika ukusanyaji wa taarifa na kurahisisha ufuatiliaji wa wahamiaji haramu. Kampeni hiyo inatarajiwa kuwa endelevu katika shehia zote za Mkoa wa Kusini Unguja.

Sheha wa Shehia ya Uroa, Adam Muhsin Amour, alitoa pongezi kwa Idara ya Uhamiaji kwa kutoa elimu hiyo muhimu, hasa kwa kuzingatia kuwa eneo lao ni la kitalii na lenye mchanganyiko mkubwa wa watu. Alisema elimu hiyo itasaidia sana katika utambuzi wa wahamiaji haramu, ufahamu wa taratibu za uraia, pasipoti na biashara haramu ya binadamu.

Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji waliungana na wananchi wa kijiji cha Uroa katika mwendelezo wa kampeni ya “Mjue Jirani Yako”, wakitoa mada mbalimbali kwa lengo la kuelimisha na kuhamasisha ushirikiano wa pamoja katika kulinda usalama na amani ya nchi na miongoni mwa mada zilizo wasilishwa ni kuhusu uraia,nani mgeni,passport na biashara haramu ya binadamu.