Na: Nishan Khamis – Zanzibar
Katibu wa Kamati ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Ndugu Khamis Mbeto Khamis, amewahimiza vijana wa hamasa wa chama hicho kutumia mitandao ya kijamii kama nyenzo muhimu katika harakati za kukea masuala ya uzushi katika na kuelezea hususani mafanikio ya viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika kikao maalum na wawakilishi wa makundi ya hamasa Zanzibar, kilichofanyika katika ukumbi wa Bububu Fuji, Wilaya ya Magharibi A, Unguja, Mbeto alisema mitandao ya kijamii ni jukwaa sahihi kwa vijana kufanikisha kazi ya kutetea chama, kukemea upotoshaji na kushiriki katika mijadala ya maendeleo ya taifa.
“Ni muhimu vijana kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi madhubuti wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mbeto.
Mbeto pia alitoa salamu za pongezi kutoka kwa Dkt. Mwinyi kwa vijana hao, akiwashukuru kwa uzalendo wao na juhudi wanazozifanya katika kukitumikia chama na taifa kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa vijana kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura, ili siku ya uchaguzi kura zote ziende kwa wagombea wa CCM, kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola.
Wataalam wa masuala ya mawasiliano kutoka Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar, Suleiman Mafuru na Haji Nyanya, walieleza kuwa siasa za kisasa zinahitaji matumizi ya mitandao ya kijamii, na kuwashauri vijana kuitumia vizuri kwa ajili ya kujinufaisha kielimu, kiuchumi, na kisiasa.
Kwa upande wao, vijana waliohudhuria mkutano huo walitoa shukrani kwa hatua ya kuwakutanisha pamoja, wakisema imeonesha mshikamano na upendo. Waliahidi kuwa Oktoba, siku ya uchaguzi, watatoa kura zao zote kwa viongozi wa CCM wakiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya nchi.
