Popular services

TAASISI YA THE GOOD HOPE SOCIETY YATOA MSAADA WA MAVAZI KIJIJI CHA KUREKE, KIJINI.



Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja

Taasisi binafsi ya The Good Hope Society imetoa msaada wa mavazi kwa wakazi wa kijiji cha Kureke, kilichopo katika shehia ya Kijini, wilaya ya Kaskazini A, Unguja.

Akizungumza na wanakijiji hao, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Ibrahim Abdul Aziz Naisha, alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikijihusisha na kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu. Alieleza kuwa lengo la ziara yao ni muendelezo wa jitihada zao za kuisaidia serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

Naisha aliwataka wakazi wa kijiji hicho kuupokea msaada huo kwa mikono miwili, huku akiwaomba kuendeleza ushirikiano na taasisi hiyo katika juhudi za maendeleo ya kijiji na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji  wa taasisi hiyo  Dkt. Seif Bakar Zubeir , alisema kuwa baada ya kufanya utafiti wa kina, walibaini umuhimu wa kutoa msaada wa mavazi kwa jamii hiyo. Alieleza kuwa jumla ya nguo 250 za wanawake, 177 za wanaume na 120 za watoto wadogo zilitolewa kwa wanakijiji hao ili kuwasaidia katika mazingira yao ya maisha.

Aidha, Dkt. Seif alisisitiza kuwa msaada huo si wa mwisho, bali ni mwanzo wa mfululizo wa misaada mingine ambayo taasisi hiyo itaendelea kutoa kadri watakavyopata fursa, kutokana na mahitaji makubwa yaliyoonekana katika kijiji hicho.

Alitoa wito kwa taasisi na wadau wengine kushirikiana ipasavyo katika kusaidia watu wenye mahitaji maalum na jamii masikini, ili kwa pamoja kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Sheha wa shehia ya Kijini, Katibu wa sheha huyo, Abdalla Makame Mkali, alisema kuwa wamepokea msaada huo kwa furaha na shukrani tele, na kwamba msaada huo ni sehemu muhimu ya mahitaji yao. Alitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia kijiji hicho katika maeneo mengine kama vile mavazi, chakula, na ujenzi wa barabara kuu ambayo ni muhimu kwa maendeleo yao.

Kwa upande wao, wananchi wa kijiji hicho walielezea furaha yao na kutoa shukrani kwa taasisi hiyo. Walisema msaada huo utawasaidia wao pamoja na watoto wao katika kujisitiri, huku wakiiomba taasisi hiyo kuendeleza juhudi hizo.

Pamoja na hayo, walitaja changamoto ya ukosefu wa kisima cha maji safi kwa baadhi ya maeneo ya kijiji hicho, na ujenzi wa barabara kubwa ya kuunganisha kijiji hicho, wakiiomba serikali kulipa suala hilo kipaumbele.