Popular services

SMZ YAJIDHATITI KUHIFADHI MAZINGIRA KUPITIA UPANDAJI WA MITI NCHI.


Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amezitaka taasisi zinazohusika na uhifadhi wa mazingira kuandaa mpango maalum wa kuhakikisha miti inayopandwa inasimamiwa ipasavyo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuirejesha "Zanzibar ya Kijani".

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika hafla iliyofanyika Chaani Masingini, Wilaya ya Kaskazini A, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Harusi Said Suleiman, amesema miti ni rafiki wa binadamu na hivyo ni muhimu kuipanda kwa lengo la kujilinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti holela na ujenzi usiofuata mipango bora umechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa uzalishaji wa chakula, hali iliyosababisha uhaba wa matunda na pengo la miti ya asili.

Ameeleza kuwa Serikali imeanzisha mpango wa upandaji miti katika eneo la Chaani Masingini baada ya eneo hilo kuteuliwa kuwa la hifadhi, likiwa pia na malengo ya kuongeza uzalishaji wa chakula. Aidha, amewatahadharisha wakulima wanaong’oa miti kwa ajili ya kilimo kuacha tabia hiyo kwani inaathiri juhudi za kuhifadhi mazingira.



Vilevile, ametoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kuendeleza utunzaji wa mazingira pamoja na kudumisha amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Nd. Ali Khamis Juma, amesema eneo la Chaani Masingini lenye ukubwa wa hekta 428 ni miongoni mwa mashamba sita yaliyotengwa kwa ajili ya upandaji wa miti — matano yakiwa Unguja na moja Pemba.

Ameeleza kuwa miti iliyokwisha pandwa katika eneo hilo ni pamoja na Mikeshia 2,500, Mivinje 2,500, Mitondoo 600, Midimu 250, Milimau 500, Mifenesi na Michungwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula nchini. Aidha, amesisitiza kuwa licha ya kuongezeka kwa matumizi ya nishati mbadala, bado ipo haja ya kuongeza kasi ya upandaji miti kila mwaka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Matar Zahour Masoud akitoa salamu za mkoa , amesema kuwa kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya watahakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa ipasavyo ili idumu kwa muda mrefu. Amewataka wananchi, hususan vijana, kuitambua na kuienzi dhana ya upandaji miti kama njia ya kulinda mazingira na kurithisha rasilimali hizo kwa vizazi vijavyo.

Siku ya upandaji miti kitaifa huadhimishwa kila mwaka tarehe 16 Aprili, ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu ni: "Zanzibar ya Kijani Inawezekana — Shiriki Kupanda na Kutunza Miti."