Popular services

SISTER ISLAND YAKABIDHI KISIMA CHA MAJI NA KUTOA MSAADA WA MAVAZI MJIMWEMA - MATEMWE, WANAKIJIJI WAFANYA SHEREHE.


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Taasisi ya Sister Island yenye makao yake Nungwi, leo imekabidhi rasmi kisima cha maji safi pamoja na msaada wa mavazi kwa wakazi wa kijiji cha Mjimwema, kilichopo kijini Matemwe, wilaya ya Kaskazini A, Unguja.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Mhasibu wa taasisi hiyo, Haji Moh’d Ali, alisema kuwa msaada huo ni mwendelezo wa jitihada zao katika kusaidia jamii zenye changamoto mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora mijini na vijijini.

Haji alisema mara baada ya kupokea taarifa za uhaba wa maji katika kijiji hicho, taasisi yao iliona ni muhimu kuchukua hatua haraka ili kuwaondolea adha hiyo wananchi. Alibainisha kuwa kwa Sister Island, kila changamoto inayojitokeza katika jamii huonekana kama fursa ya kuleta mabadiliko chanya.

Aidha, kwa niaba ya Mkurugenzi wa taasisi hiyo, alitoa shukrani kwa ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa wanakijiji hadi kukamilika kwa mradi huo, na kuwaomba waendelee kushirikiana nao ili kuweza kukabiliana na changamoto nyingine zitakazojitokeza kwa maendeleo ya pamoja.

Kwa upande wake, Mratibu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Mkasi Hassan Thabit, alitoa pongezi kwa Sister Island kwa juhudi zao katika kuleta maendeleo, hususan katika sekta ya huduma za kijamii. Alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika ushirikiano na serikali na ameahidi kuendeleza mashirikiano hayo kwa manufaa ya wananchi.

Nao  baadhi ya viongozi  akiwemo Naibu Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya hiyo, Twalib Haji Abas, pamoja na Diwani wa Viti Maalum kutoka kundi la watu wenye ulemavu, Bi Fatma Mngwali, waliipongeza taasisi hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa misaada mbalimbali. Wameahidi kuendelea kushirikiana nao kwa lengo la kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Viongozi hao pia waliwasihi wanakijiji kukitunza kisima hicho na kukitumia kwa njia sahihi, ikiwemo kuanzisha shughuli za kilimo cha umwagiliaji, ili kuongeza uzalishaji wa mboga mboga na mazao mengine kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Wanakijiji nao waliungana kutoa shukrani kwa Sister Island, wakisema kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya muda mrefu ya maji, hasa wanawake, hivyo kisima hicho kimekuwa faraja kubwa kwao pamoja na msaada mavazi . Waliahidi kukitunza vizuri na kuendeleza ushirikiano wao na taasisi hiyo kwa maendeleo endelevu ya kijiji chao.