Popular services

SISTER ISLAND YAKABIDHI AMBULANSI KITUO CHA AFYA KENDWA, WANANCHI WASHUKURU


Na Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Taasisi ya Sister Island iliyopo Nungwi leo imekabidhi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kwa kituo cha afya cha binafsi cha Kendwa Maternity Clinic, kwa lengo la kuwasaidia wakazi wa jimbo la Nungwi, hasa wanawake waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya usafiri wa dharura kwa muda mrefu.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano kwa niaba ya Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mhasibu wa Sister Island, Haji Moh’d Ali alisema waliitikia ombi kutoka kwa uongozi wa kituo hicho pamoja na wanajamii, na kwa kushirikiana na wafadhili kutoka Italia, waliamua kutoa msaada huo ili kuondoa adha ya usafiri kwa wagonjwa.

Haji alisema kuwa kwa niaba ya uongozi wa Sister Island, wanafurahia kufanikisha zoezi hilo na wamepokea mapokezi chanya kutoka kwa jamii na uongozi wa kituo, jambo linaloonesha nia ya kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali. Aliwataka wananchi kuitunza ambulansi hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Twalib Haji Abas aliipongeza taasisi hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya, na kuzihimiza taasisi nyingine kuiga mfano huo. Pia aliwasihi wananchi kuendeleza ushirikiano na wawekezaji ili kunufaika zaidi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Sheha wa Shehia ya Kilindi, Ibrahim Maabad Juma, alisema ujio wa gari hiyo katika jimbo la Nungwi, hasa katika shehia yake, ni mkombozi mkubwa kwa kuwa walikuwa wakikumbwa na matatizo ya usafiri wa wagonjwa, hasa kuwapeleka Hospitali ya Kivunge. Aliahidi kushirikiana na jamii kuitunza gari hiyo kwa manufaa ya muda mrefu, huku akiomba Sister Island waendelee kusaidia wananchi zaidi.

Daktari Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Hawa Kilembele, alisema msaada huo ulikuwa muhimu sana kutokana na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda Kivunge. Alisema mara kadhaa walilazimika kutumia zaidi usafiri binsfi  hasa nyakati za usiku, kuwapeleka wajawazito na wagonjwa wengine katika hospitali hiyo.

Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa msaada wa taulo za kike kwa wanawake wanaohudumiwa kituoni hapo, jambo ambalo limepokelewa kwa shukrani kubwa kutokana na umuhimu wake.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kendwa, Pili Musa Juma, alishukuru kwa msaada huo na kusema kuwa kwa muda mrefu walikuwa wakipata tabu, hasa akina mama nyakati za usiku, hivyo ujio wa gari hiyo ni neema kwao. Aliiomba taasisi hiyo kuendeleza moyo huo wa kusaidia jamii, hasa maeneo ya vijijini.