Na,Nishan khamis-Kaskazini Unguja.
Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni ya huduma ya kisheria ya Mama Samia, utakaofanyika siku ya Jumatano, tarehe 23 Aprili mwaka huu katika mkoa huo.
Akizungumza na masheha na watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano uliofanyika Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Bw. Khamis Bakar Amani kutoka Ofisi ya Rais - Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, ambaye pia ni Mratibu wa kampeni hiyo katika mkoa huo, amesema kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman.
Amesema kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuimarisha upatikanaji wa haki na usawa kwa wote, hususan wanawake, watoto na watu wanaoishi katika mazingira magumu. Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni: “Msaada wa Kisheria ni Haki, Usawa na Amani kwa Maendeleo ya Taifa.”
Bw. Amani amewaomba masheha kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi huo, kwani kutakuwepo na wataalamu mbalimbali wa masuala ya kisheria ambao watatoa huduma na ufumbuzi kwa changamoto zitakazoletwa na wananchi papo kwa papo.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi na Uendeshaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Bi. Mboja Hisabu Ali, amesema kwa niaba ya ofisi kuwa wamepokea kwa furaha ujio wa kampeni hiyo, kwani italeta mafanikio makubwa kwa wananchi kwa kupatiwa msaada wa kisheria juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni hiyo, na kuwataka masheha waendelee kutoa hamasa zaidi kwa wananchi ili waweze kufaidika na fursa hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Nao baadhi ya masheha waliokuwepo katika kikao hicho wamesema wamefarijika na ujio wa kampeni hiyo pamoja na elimu waliyoipata, na wameahidi kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kueleza changamoto zao na kupatiwa suluhisho.
Wamesema kuwa shehia ndiko kwenye changamoto nyingi za kisheria, hivyo kampeni hiyo imekuja kwa wakati muafaka.
