Popular services

WANANCHI WAHIMIZWA KUDUMISHA MUUNGANO NA KUWAENZI WAASISI, VIJANA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VISHAWISHI VYA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI


Na Nishan Khamis - Nungwi

Wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja wametakiwa kuendelea kushirikiana katika kudumisha umoja na mshikamano wa Muungano wa Tanzania, pamoja na kuwaenzi waasisi wa Muungano kwa kutambua jitihada kubwa walizozifanya ambazo zimeleta manufaa ya maendeleo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Khamis Mohamed Muhammad, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano yaliyofanyika katika uwanja wa mpira wa Hamburu, Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa maendeleo yanayoonekana nchini ni matokeo ya tunu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuitunza tunu hiyo na kuwaenzi waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, kutokana na juhudi zao kubwa za kuunganisha nchi hizi mbili.

Aidha, alieleza kuwa changamoto mbalimbali za Muungano zimekuwa zikitafutiwa ufumbuzi na zinatarajiwa kuendelea kutatuliwa ili kuimarisha zaidi maendeleo nchini. Alisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wananchi wanapaswa kuendelea kuwaunga mkono ili kuimarisha zaidi mafanikio ya Muungano huu.

Akizungumza katika kilele hicho, Mratibu wa Wilaya hiyo, Mkasi Hassan Thabit, alisema maadhimisho hayo yaliambatana na shamrashamra zilizoanza tarehe 21 Aprili 2025, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika Hospitali ya Kivunge na michezo mbalimbali katika maeneo ya Wilaya hiyo, kama njia ya kuonesha umuhimu wa matunda ya Muungano.

Mratibu huyo alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, upendo na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili tunu ya Muungano wa amani iendelee kudumu nchini.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya hiyo, Twalib Haji Abas, aliwasihi vijana kutambua na kuthamini Muungano, na kuwataka kuepuka kushawishiwa na watu wenye nia mbaya ya kuvuruga Muungano wenye manufaa makubwa kwa Watanzania.

Naye Mzee Makolos Habibu Haji kutoka Kijiji cha Kilimani Tazari aliwahusia vijana kusoma historia ya Muungano ili waweze kuongeza uzalendo kwa ajili ya maslahi mapana ya kudumisha amani, utulivu, na mshikamano unaotokana na tunu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.