Popular services

MBUNGE TAMIMA AWAFARIJI WAGONJWA HOSPITALI YA KIVUNGE, ATOA MKONO WA EID-AL-FITR



Na Nishan Khamis

Kaskazini Unguja

Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Tamima Haji Abas, leo amewatembelea na kuwafariji wajawazito waliolazwa na wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Kivunge. Ziara hiyo imelenga kuwapa faraja kutokana na changamoto wanazopitia pamoja na kuwapatia mkono wa Eid-al-Fitr ili waweze kusherehekea sikukuu hiyo baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Tamima alisema, kama mzazi na kiongozi, ana wajibu wa kuwafariji wanawake hao ili kuwapa matumaini na kuwahamasisha. Alisisitiza kuwa anajivunia kuona kizazi kipya cha Jeshi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikizaliwa kwa misingi ya maslahi mapana ya taifa.

Aidha, aliwapongeza akina mama hao kwa kazi kubwa ya kuleta maisha mapya duniani na aliwahimiza kuwalea watoto wao kwa misingi ya maadili mema ili kuhakikisha taifa linakuwa na kizazi chenye malezi bora kwa maslahi ya familia na nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Daktari Dhamana Msaidizi wa hospitali hiyo, Dkt. Tamimu Hamad Said, alieleza kuwa kitendo hicho ni cha kupongezwa kwani kinaonesha uongozi wa karibu na jamii. Alitoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo kwa kutembelea na kuwafariji wagonjwa na wazazi hospitalini, kwani ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika jamii.

Naye, Amina Suleiman, mmoja wa wazazi waliokuwa wodini baada ya kujifungua, alimshukuru Mbunge Tamima kwa msaada wake na moyo wa upendo aliouonesha kwao. Alisema wamefarijika sana na zawadi walizopewa, akimuombea mbunge huyo afya njema na mafanikio zaidi ili aendelee na moyo wa kusaidia jamii.