JAMII YASISITIZIWA KUWAJUMUISHA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KATIKA NAFASI ZA UONGOZI
Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Jamii imetakiwa kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha wanawake wenye ulemavu wanapewa nafasi pana katika uongozi wa kitaifa, kwani kundi hilo lina uwezo, ubunifu na mchango wa kipekee katika ustawi wa jamii. Wito huo umejidhihirisha zaidi kufuatia hatua ya Bi Ulaya Khamis Juma, mwanamke mwenye ulemavu, kutunukiwa Tuzo ya Mfanyakazi Bora hapo jana katika Ofisi ya Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja
Akizungumza na kisiwa news blog Ulaya ambaye ni Katibu wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Kaskazini A na Mjumbe wa NAPAC, amesema ameendelea kuonesha mfano wa uongozi wenye uwajibikaji, nidhamu na kujitoa kwa jamii. Kupitia nafasi yake, ameweka msukumo mpya katika kutetea haki, fursa sawa na upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu, huku akisisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi.
Hivyo ametoa pongezi za dhati na kuiomba jamii iendelee kuwaunga mkoa wanawake kwenye nafasi za uongozi kwani wanauwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo nchini.
Halikadhalika Ulaya aliwahimiza wanawake wenye ulemavu kujenga ujasiri, kuamini uwezo wao na kusimama imara kutafuta nafasi za uongozi. Alisisitiza kuwa “ulemavu si kikwazo cha mafanikio, bali ni sehemu ya safari ya uongozi kama utachochewa na juhudi na malengo makini.”Kwa upande wake Khamis Rashid Khamis, afisa wa watu wenye ulemavu wa Wilaya ya Kaskazini A, alisema kuwa mafanikio ya Bi Ulaya yanadhihirisha uwezo mkubwa wa wanawake wenye ulemavu katika majukumu ya uongozi endapo watapewa nafasi. Alisema uongozi wa mfano aliouonyesha unaendelea kuimarisha jitihada za wilaya katika kujenga jamii jumuishi na isiyomuacha mtu nyuma.
Naye Farihia Abdalla Juma, Mwanaharakati wa Haki za Wanawake na Katibu wa Jukwaa la Wanawake Kaskazini Unguja, alisema Bi Ulaya amekuwa nguzo muhimu ya kuhamasisha wanawake wenye ulemavu kujitokeza kwenye nafasi za maamuzi. Alieleza kuwa mafanikio hayo yanafungua ukurasa mpya wa matumaini katika mapambano ya uwezeshaji wa wanawake nchini.
