Waumini wa dini ya Kiislamu mkoa wa Kaskazini Unguja wamehimizwa kuwalea watoto katika malezi na maadili mema, pamoja na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia matendo mema na kudumisha amani na utulivu ambao ni msingi wa maendeleo ya dini na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wilaya ya Kaskazini B, Juma Mmanga, alipofungua Itikafu ya siku tatu katika Msikiti Nasri Matemwe Mnazi Mrefu, wilaya ya Kaskazini A, kwa niaba ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar.
Amesema kuwa ibada ya itikafu ni fursa adhimu ya kujenga imani, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuacha yale aliyokataza sambamba na kutekeleza aliyoyaamrisha jambo ambalo ni msingi wa kufaulu hapa duniani na Akhera. Mmanga amewahimiza waumini kuendeleza matendo mema kwa maslahi ya maisha ya sasa na baadaye.
Aidha, amewataka wananchi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilika kwa uchaguzi mkuu kwa salama na amani, akisema ni historia muhimu kwa taifa. Pia amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendeleza uongozi unaojikita katika umoja, ushirikiano, amani na utulivu misingi iliyoleta maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa waumini na jamii kwa ujumla kuendelea kutunza amani, kudumisha utulivu na kushirikiana kuendeleza maendeleo ya dini na taifa.
Akisoma risala katika hafla hiyo, Amiri Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiislamu Matemwe, Sheikh Kundi Chumu, alisema kuwa itikafu hiyo ni ya tano tangu kuanzishwa kwake na wazee wa Matemwe, ikiwa na lengo la kuwalea watoto katika maadili ya Kiislamu na kuwaepusha na mila na desturi zisizofaa za kimagharibi, hususan kipindi cha sikukuu ambapo vijana wengi hujihusisha na hanasa zinazoharibu utamaduni wa Kiislamu.
Aidha, aliipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na watendaji wake kwa uongozi wa unyenyekevu na kusikiliza changamoto za wananchi, akisema ni mfano wa kuigwa. Aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana katika kulinda amani na utulivu nchini.
Baadhi ya waumini waliohudhuria itikafu hiyo akiwemo Amir Shaib Juma na Mashatali Juma walisema kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu iliyosisitizwa sana katika Uislamu, hivyo ni wajibu wa waumini kuilinda kwa ajili ya ustawi wa dini na jamii. Walihimiza waumini wengine kujitokeza kushiriki itikafu kwa manufaa ya maisha ya dunia na Akhera.
