Na, Nishan Khamis – Zanzibar
Katika kijiji cha Kinduni Kichungwani, Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja, mwaka 1981 amezaliwa mtoto wa kike ambaye amekuwa miongoni mwa wanawake wanaoandika historia katika uongozi, elimu ya juu na siasa za Zanzibar. Huyu ndiye Mboja Ramadhan Mshenga, mama wa watoto watatu wa kike, kiongozi, msomi, na mwanamke ambaye safari yake imejaa ushindi dhidi ya changamoto, kujitoa na kuamini katika nguvu ya elimu ,uvumilivu na utumishi kwa jamii ni siri ya mafanikio.
Akiwa msichana mdogo, Mboja amesema hakujua kwamba kukaa kwenye mikutano ya chama katika uwanja wa Mshikamano Kijangwani kulikuwa kunamjengea msingi wa maisha yake ya baadaye amabpo alivutiwa na mijadala, nyimbo, hamasa na matukio makubwa ya kisiasa aliyoshuhudia wakati huo. "Kila tukio lilichochea ndani yangu mbegu ya uongozi,mbegu ambayo imetokea na kuwa mti mkubwa wenye matunda ya busara, ujasiri na uzoefu"amesema Mboja.
Safari yake ya elimu ilianza mwaka 1989 katika Skuli ya Muembe Shauri, kisha Kajificheni alikomaliza 1995,alijiunga na Hamamni Sekondari mwaka 1996, na amemaliza Kidato cha Nne skuli ya Kidongo Chekundu mwaka 2000. Kwa imani kwamba elimu ndiyo ufunguo wa maisha, "nilirudia mitihani 2002 na 2007 kupitia Ben Bella Centre, hatua hizi ndizo zilizonifikisha hadi IPS Chanika ambako nilisomea masomo ya manunuzi na hatimaye kupata Cheti 2009 na Diploma 2011" Amesema Mboja.
Uamuzi wake wa kusonga mbele ulimfikisha NIT Dar es Salaam, akapata Shahada ya Procurement and Logistics Management (2014–2017), kisha akaendelea kusoma Master’s ya Umahiri katika Ujasiriamali na Ubunifu kupitia Chuo Kikuu cha Mzumbe (2020–2022). Mwaka 2024 akaanza ngazi ya juu zaidi PhD katika Innovation and Entrepreneurship Management kupitia Nelson Mandela African Institution of Science and Technology, Arusha.
Mboja, kila ngazi ya elimu ilikuwa ni ushindi wa binafsi, ushindi wa familia yake, na ushindi kwa wanawake wanaotamani kupanda ngazi bila kujali vikwazo.
Katika uongozi wa kisiasa, Mboja hakutokea ghafla, alijengwa na mazingira, watu na muda alipata kadi yake ya uanachama mwaka 2000 akiwa anamaliza kidato cha nne, lakini roho ya siasa ilishaiva ndani yake tangu utotoni. "Nilianza kama mwanachama wa kawaida, nikapanda kuwa Katibu wa Maskani, kisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu UWT Tawi la Wendapole Welezo".amesema.
Safari ikaendelea hadi kuwa Mjumbe wa Sheha, Msimamizi wa Kituo cha Uchaguzi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya Kaskazini B, Mjumbe wa Baraza Kuu Wazazi Taifa, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Mkoa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa, na Mjumbe wa Halmashauri ya Jimbo la Mahonda mwaka 2022.
Suleiman Haji ‘Kisube’, rafiki yake wa siku nyingi, amesema "tangu akiwa mtoto alimwona Mboja akiwa na shauku ya uongozi, hasa siasa" Amesema. Hivyo amekuwa akijihusisha kwake mapema na uongozi wa vijana kulimjenga, na hatua alizofikia leo ni matokeo ya maandalizi na subira za muda mrefu. Kwa mujibu wake, Mboja ni msikivu, mbunifu, mchapa kazi na mwenye misimamo kielelezo cha uongozi kwa wanawake wa Zanzibar.
Kwa upande wa chama, Ahmada Vuaa Shaa, Mwenezi wa Siasa, Itikadi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, amesema wanawake wawili kuchukua majimbo katika Mkoa huo ni hatua kubwa ya usawa wa kijinsia. Anaamini uwepo wa Mboja katika Jimbo la Mahonda ni mwanzo wa misingi mipya ya siasa shirikishi ambayo ndio sera ya chama hicho."chama kinatambua uwezo wake wa kiuongozi, ndiyo maana dhamana aliyopewa imewekwa sehemu salama katika mikono ya mtu mwenye weledi, uadilifu na dhamira ya kuwatumikia wananchi na kumuunga mkono Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi" Amesema Ahmada.
Mbali na siasa, Mboja ametoa mchango mkubwa serikalini kupitia Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST) alikohudumu karibu miaka 10 kama Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Uondoaji wa Mali za Umma. Alisimamia rasilimali za umma kwa weledi na uadilifu, akijenga rekodi inayotambuliwa na wengi.
Na sasa, katika kilele cha safari yake ya utumishi, Mboja Ramadhan Mshenga ni mwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi kutoka jimbo la Mahonda na ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, uteuzi unaotazamwa na wengi kama uthibitisho wa uwezo wake, uaminifu wake na mchango mkubwa anaotarajiwa kuupeleka katika sekta muhimu kwa uchumi wa taifa.

