Popular services

SKULI YA MAMA AFRICA YAFANYA MAHAFALI, WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO.


Na, Nishan Khamis – Nungwi.
 jamii imetakiwa kutoa ushirikiano wa karibu baina yao na walimu katika kusimamia maadili ya wanafunzi ili kuhakikisha elimu inaendelea kupiga hatua na kufikia mafanikio katika ngazi ya msingi.

Akizungumza katika mahafali ya tisa ya darasa la saba ya Skuli ya Mama Africa Children Care Association huko Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Makame Ramadhani Mbanji, alisema ili kufikia misingi na mitaala ya kielimu iliyopo, wazazi wanatakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa watoto wao ili kupata matokeo bora katika elimu ya msingi. Alisisitiza haja ya kuhakikisha watoto wanapata walimu wenye uwezo na weledi utakaowajengea uelewa sahihi na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu kwa maslahi ya maendeleo ya watoto na taifa kwa ujumla.
Aidha, aliipongeza skuli hiyo kwa kufanya vizuri katika ufundishaji na kuwa miongoni mwa skuli zinazofanya vizuri katika wilaya na mkoa huo. Alisisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili kwa watoto, akibainisha kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano kati ya wazazi na jamii ili kujenga taifa lenye vijana wazalendo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa skuli hiyo, Lucy John Mpembo, alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwa ushirikiano wa walimu, wazazi na walezi ili kuhakikisha jukumu la elimu linafanikiwa ipasavyo.
Lucy amewataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu pamoja na kamati za skuli kwa kuhudhuria vikao vya mara kwa mara na kufuatilia maendeleo ya watoto ili kuwaongoza vyema katika kutimiza malengo yao ya maisha kwa maendeleo ya familia na taifa.
Akiwasilisha risala ya wanafunzi, Mwashamba Mussa Ali alisema skuli yao inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa madarasa, kutoshirikishwa katika makongamano ya kukuza vipaji, talaka na mifarakano ya wazazi inayoathiri watoto, vitendo vya udhalilishaji na ukatili vinavyoathiri kujiamini kwa watoto, pamoja na ukosefu wa uzio wa kuzunguka skuli kutokana na mazingira ya eneo hilo.

Naye Afisa Polisi wa Kituo cha Nungwi, Zauda Juma Ibrahim, aliwasisitiza wazazi na walezi kuwa makini na watoto kipindi hiki cha kuelekea likizo, kwa kuwakinga dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili, sambamba na kuwa makini na usalama wa barabarani kutokana na ongezeko la ajali katika jamii.