Na, Nishan Khamis-Mkokotoni.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kaskazini A imezitaka jamii kuendelea kushirikiana kikamilifu katika kuimarisha ulinzi na amani, hasa katika kipindi hiki ambacho maeneo ya bandari zisizo rasmi yanahitaji uangalizi wa karibu ili kudhibiti uingiaji holela unaoweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini. Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Rashid Simai Msaraka, alipokuwa akizungumza na masheha, kamati za bandari, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa madiko pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili na kudhibiti viashiria vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Amekumbusha kuwa ni marufuku kwa majaazi yenye leseni ya kubeba mizigo kubeba abiria, na kwamba yeyote atakayebainika kukiuka sheria atalazimika kuchukuliwa hatua stahiki. Aidha, amewataka masheha kuwasilisha ripoti za kila wiki kuhusu hali ya ulinzi katika maeneo yao, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa wahamiaji haramu.
Pia amehimiza mashirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama katika doria zinazoendelea katika wilaya hiyo, huku akieleza kuwa wilaya hiyo ipo salama kabla na baada ya uchaguzi jambo ambalo amewataka wananchi kuendeleza tunu ya amani nchini na kuepukana na vishawishi vya kudhohofisha tunu hiyo.
Kwa upande wake, mkuu wa bandari ya Mkokotoni, Khamis Khamis, amesema ameshukuru kwa uwepo wa kikao hicho kwani kwa upande wa bandari ya Mkokotoni, mikakati madhubuti kudhibiti uingiaji wa watu kiholela, huku akisisitiza kuwa maadhimio ya kikao hicho anayafanyia kazi ipasavyo kwa maslahi mapana ya wilaya na taifa kwa ujumla.
Naye Sheha wa Shehia ya Pitanazako, Acheni Machano Juma, amesema elimu aliyoipata na malengo ya kikao hicho atahakikisha anayachukua na kuyafanyia kazi ipasavyo na kuwaeleza jamii katika kudhibiti wahamiaji haramu katika maeneo ya shehia yake na amewasisitiza wananchi kutoa taarifa za wahamiaji haramu wanaoingia katika maeneo yao.
