NA FAUZIA MUSSA
WAKALA wa Chakula na Dawa (ZFDA) umewataka wagonjwa, wanafamilia na wataalamu wa afya kuripoti madhara yeyote yanayoshukiwa kutokana na dawa ili kusaidia kuwalinda wengine.
"Unaporipoti madhara ya dawa umesaidia kumlinda mwengine, si madaktari, wafamasia au wasimamizi pekee bali kila mmoja ana jukumu hilo" alisema Mkurungezi Mtendaji ZFDA, Dk. Burahan Othman Simai katika taarifa aliyoitoa kwa umma katika wiki ya usalama wa dawa.
Dk. Burahan aliwasisitiza wagonjwa, wanafamilia, wauguzi, madaktari na wataalamu wengine wa afya kutumia mfumo wa uangalizi wa usalama wa dawa (pharmacorvigilance) unaopatikana kwenye tovuti ya ZFDA au kutumia programu ya simu ya ZFDA PV katika kuripoti madhara hayo.
Alieleza kuwa taarifa zote zitakazowasilishwa kwa wakala hao zitachunguzwa kwa kina na kuchukuliwa hatua stahiki ili kulinda afya na usalama wa watumiaji wa dawa.
"ZFDA kama mamlaka nyengine za udhibiti wa dawa imeanzisha mifumo ya kuripoti na kufuatilia usalama wa dawa ili kusaidia kukusanya taarifa zaidi kuhusu madhara yanayojulikana na yale yanayobainika kuwa ni mapya, hali hii itasaidia kuchukuliwa hatua kama kutolewa tahadhari za usalama na mabadiliko ya matumizi." alisema
Katika taarifa hiyo Dk. Burahan alieleza kuwa dawa huokoa maisha na kuimarisha afya za watu, hata hivyo wakati mwengine zinaweza kusababisha madhara yasiotarajiwa na kuisisitiza jamii kutoa taarifa pale madhara yanapojitokeza ili mamlaka za udhibiti zichukue hatua.
"Tafiti zinaonesha kuwa madhara yanayoshukiwa huripotiwa takribani kwa asilimia 5-10" alisema Dk. Burhan katika taarifa hiyo
Taarifa ilieleza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa mwamko wa kuripoti matukio hayo bado ni mdogo na kueleza kuwa wiki ya usalama wa dawa inalenga kuhamasisha jamii kuripoti na kufahamu umuhimu wa kutoa taarifa.
"Watu wengi hawaripoti madhara ya dawa kutokana na kutokujua kama zinaweza kuleta madhara au kutoona umuhimu wake, kupitia wiki hii tunaongeza uelewa kuhusu umuhimu, wapi na jinsi ya kuripoti madhara yanapotokea " alisema Dk.Burhan
Wiki ya usalama wa dawa huadhimishwa kuanzia novemba 3-9 kila mwaka tangu kuanzishwa mwaka 2016 duniani ambapo Zanzibar imeanza kuadhimisha wiki hiyo 2021 ambapo kwa mwaka huu wiki hiyo imebeba ujumbe "Kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha usalama wa dawa kwa kuripoti madhara yanayoshukiwa kutokana na dawa. Mimi na wewe tunaweza kusaidia kufanya matumizi ya dawa kuwa salama zaidi kwa wote."
MWISHO

