Popular services

WANANCHI JIMBO LA KIJINI WAMFAGILIA BADRIA, WAAHIDI KUMPA USHIRIKIANO

 

Na Nishan Khamis, Zanzibar

Wananchi wa Jimbo la Kijini, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamesema wanajivunia kuchaguliwa  Badria Attai Masoud kuwa Mwakilishi wa jimbo hilo na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, wakieleza kuwa hatua hiyo imeleta hamasa mpya kwa jamii hasa wanawake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema uteuzi huo umeonesha uthubutu wa mwanamke kuingia katika nafasi za juu za uongozi na kuwapa matumaini makubwa ya utatuzi wa changamoto zinazolikabili jimbo hilo, ikiwemo miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji safi na salama, miundombinu ya skuli, pamoja na huduma za uwezeshaji kwa vijana na wanawake.

Juma Machano Haji, mkazi wa Shehia ya Kivunge, amesema jimbo hilo limeweka historia kwa kupata kiongozi mwanamke baada ya muda mrefu kuongozwa na wanaume, hatua ambayo imeonesha wazi uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

“Badria ameweka historia katika jimbo letu tangu kura za maoni hadi uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Ni mwanamke wa kwanza kuwa Mwakilishi wa jimbo letu na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri. Tunajivunia,” alisema Machano.

Ameongeza kuwa wataendelea kumpa ushirikiano mkubwa na kuhamasisha jamii kuwaamini wanawake katika nafasi za uongozi kwa kuwa wana uwezo, maono mapana na uthubutu wa kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja, pamoja na mwanaharakati wa masuala ya wanawake na uongozi, Farihia Abdalla Juma, amesema mkoa huo una majimbo nane na wadi 17, na hatua ya Badria kuwa Mwakilishi na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar ni jambo la kutia moyo na linaendelea kuvunja mifumo dume katika nafasi za uongozi.

Ametoa wito kwa mashirika, jamii na taasisi mbalimbali kuendelea kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza kuwania nafasi za uongozi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Nae Badria Attai Masoud ameishukuru jamii ya Kijini kwa imani na mapokezi mazuri waliyompa, sambamba na kuahidi uongozi wa karibu, uwazi na ushirikiano wa kudumu na wananchi.

Amesema huduma za kijamii, uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na miundombinu ya usafiri na ujenzi vitapewa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo yenye tija na ufanisi.

Badria pia amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, akisema uteuzi huo ni heshima kubwa na utamfanya afanye kazi kwa bidii zaidi kwa manufaa ya wananchi wa Kijini na Zanzibar kwa ujumla.

“Wito wangu kwa jamii ni mmoja tu,tushirikiane kwani  maendeleo hayaji bila umoja, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi kwani tukisimama pamoja, Kijini na Zanzibar vitapiga hatua kubwa zaidi,” amesema.