Popular services

UMASAKA WAJUMUIKA NA WATOTO YATIMA KATIKA IFTAR YA PAMOJA

Na,Nishan khamis. 

Wilaya ya kaskazini A Unguja. 

Umoja wa Makundi ya Sanaa Wilaya ya Kaskazini A Unguja (UMASAKA) leo umeandaa iftar ya pamoja na watoto yatima zaidi ya 30, pamoja na walezi wao na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo.

Akizungumza baada ya iftar, Mwenyekiti wa UMASAKA, Mustapha C. Markus, amesema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kushiriki na watoto hao, kwani ni jambo jema lenye faida kubwa, hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kuwa karibu na makundi haya ili kuwafariji na kuwafanya wajihisi kama watoto wengine.

Aidha, Markus amewahimiza watoto hao kujitahidi katika masomo yao, kuwa na nidhamu, heshima, na bidii ili kufanikisha malengo yao maishani. Pia, ametoa pongezi za dhati kwa Afisa Utamaduni wa wilaya hiyo na timu nzima ya UMASAKA kwa kushirikiana kwa hali na mali kufanikisha tukio hilo.

 Amesema kuwa hii ni hatua ya mwanzo tu, na ametoa wito kwa wasanii wenzake kuendelea kumuunga mkono ili kufanikisha malengo makubwa ya wasanii katika wilaya hiyo.

Kwa upande wao, watoto waliokuwepo kwenye hafla hiyo wamesema wamefarijika kwa tukio hilo, kwani limewapa matumaini na faraja. Wameomba dua kwa Umoja wa UMASAKA ili uendelee kuimarika, huku wakiahidi kufanyia kazi nasaha walizopewa kuhusu elimu ya madrasa na skuli ili wakue katika maadili mema na kufanikisha malengo yao ya maisha.