Na,Hamisi Nishani, Zanzibar.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi Tanzania mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya watu 1,889,773, ambapo wanaume ni 915,492 (asilimia 48.4), huku wanawake wakiwa 974,281 (asilimia 51.6). Pamoja na kuwa wanawake wanaunda sehemu kubwa ya idadi ya watu Zanzibar, tafiti zinaonesha kuwa wao pia wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU). Ripoti mbalimbali za afya zinaonesha kuwa wanawake wanapata maambukizo ya VVU mara mbili zaidi ya wanaume. Hali hii inatokana na sababu kadhaa za kijamii, kiuchumi, na kibaolojia zinazoathiri uwezo wao wa kujilinda dhidi ya maambukizi.
Mwanaharakati wa masuala ya UKIMWI Zanzibar, Dkt. Sihaba Saadat, amesema kwa mujibu wa tafiti za Tume ya Taifa ya UKIMWI, imeonesha kuwa jumla ya watu 60,000 mwaka 2023 wanapata maambukizo mapya ya VVU Zanzibar, ambapo wanawake wanapata maambukizo mara mbili zaidi ya wanaume, yaani 42,000 kwa wanawake na 18,000 kwa wanaume. Dkt. Saadat amesema miongoni mwa sababu za ongezeko la VVU ni pamoja na watu kuwa na wapenzi wengi zaidi ya mmoja, kuanza ngono katika umri mdogo, ambapo tafiti zinaonesha wasichana wengi huanza ngono kati ya miaka 15 hadi 24, biashara ya miili kwa wanawake, kufanya ngono isiyo salama, pamoja na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.
Hali hii imekuwa tete visiwani Zanzibar kwani, kwa mujibu wa takwimu kutoka Tume ya UKIMWI Zanzibar 2023, zinaonesha kuwa asilimia 0.4 ya wakaazi wa Zanzibar wanaishi na VVU, ambapo mkoa wa Kusini Unguja unaongoza ukiwa na asilimia 0.8, Kaskazini Unguja asilimia 0.7, Mjini Magharibi asilimia 0.4, Kaskazini Pemba asilimia 0.2, na Kusini Pemba asilimia 0.5.
Daktari Sharif Haji Shehe kutoka Kituo cha Huduma na Tiba ya Hospitali ya Wilaya ya Kivunge amesema virusi vya UKIMWI vinachochewa na njia mbalimbali za maambukizi, zikiwemo kufanya ngono isiyo salama, matumizi ya kuchangia vitu vyenye ncha kali, na kupitia michubuko au vidonda vya mtu mwenye VVU. "Dalili za mtu mwenye VVU ni kama vile kupungua uzito mwilini, kifua kikuu (TB), kuharisha na kutapika sugu pamoja na majipu na vidonda visivyopona katika mwili," alieleza.
Dkt. Sharif alisema, "Mara baada ya mtu kufika na dalili hizo, anapaswa kwenda kituo cha afya kwa ajili ya kupima VVU. Ikiwa atagundulika kuwa na VVU, anapaswa kuanza matibabu ya ARVs (dawa za kupunguza makali ya VVU), kujiimarisha na lishe bora, kuchukua tahadhari ili kuzuia kueneza maambukizi, na kupata ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia."
Aidha, Dkt. Sharif ametoa wito kwa jamii kuondoa unyanyapaa na ubaguzi, kuwaelimisha watu kuhusu VVU na UKIMWI, kuwapa msaada wa kijamii na kihisia watu wenye VVU, na kuhamasisha watu kupima na kujikinga. Katika kupambana na janga hili.
kwa mujibu wa chapisho la mtandaoni la gazeti la Nipashe la tarehe 21 Septemba 2024, Serikali ya Zanzibar imetenga jumla ya Sh. bilioni 33.4 kwa ajili ya kuisaidia Tume ya UKIMWI kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI na kufuatilia makundi maalumu, ikiwemo vijana, kuona kwamba yanadhibitiwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harun Said Suleiman, alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani. Waziri Suleiman alisema Tume hiyo imepewa majukumu mengi, ikiwemo kuhakikisha maambukizi yanayotokana na ugonjwa huo yanapungua kwa kiasi kikubwa. Alitaja mikakati mingine ikiwemo kutoa elimu ya kupambana na UKIMWI kupitia makundi mbalimbali hatarishi ambayo yanaongoza kwa maambukizi mapya.
Akitoa takwimu, Waziri Suleiman alisema maambukizi mapya yamepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia mwaka 2005, mwaka ambao Serikali ilianzisha huduma za matibabu kwa waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI, ikiwemo kuwapatia dawa watu wanaoishi na VVU. Alisema kwa miaka minne iliyopita, maambukizi ya ugonjwa huo yamepungua kutoka watu 519 waliopata maambukizo mapya kwa mwaka 2020 hadi 362 kwa mwaka 2023. Aliongeza kwamba, kwa mwaka 2024 hadi kufikia Julai, watu 213 waligundulika na maambukizo mapya ya VVU, na tayari wanatumia dawa za kufubaza maradhi hayo.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar, katika kufanya uchechemuzi wa utoaji wa elimu ya masuala ya afya ya uzazi na UKIMWI, imewapatia elimu hiyo wahabari 27 Unguja ili kutumia kalamu zao kuisaidia jamii. Khairat Ali, afisa mawasiliano TAMWA-ZNZ, alisema vyombo vya habari vina msaada mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini, hivyo kupitia mafunzo waliyopewa, wanahabari wataweza kufanya uchechemuzi katika jamii kuhusu masuala ya afya ya uzazi na VVU.
NAe,mwenyekiti wa bodi ya jumuiya ya watu wanao ishi na virus vya UKIMWI Zanzibar (Zapha+) Hasina Hamad Shehe, amesema "bado suala la unyanyapaa, ubaguzi wa kutisha kwa watu wanao ishi n VVU Bado upo katika jamii ambao unakwanza jitihada zao hivyo ni lazima ushirikiano wa pamoja unahitajika katika kuelimisha jamiii juu ya watu wanao ishi na virus vya VVU ili kufikia malengo ya dunia ya kuondokana na maradhi hayo".
Ngwali Hussein Ame na Asma Ali Makame kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamesema suala la maradhi ya UKIMWI linapaswa kutiliwa mkazo, na kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha juhudi za elimu na uhamasishaji kuhusu mbinu za kujikinga, pamoja na kuhimiza usawa wa kijinsia katika maamuzi yanayohusu afya ya uzazi, Serikali, mashirika ya afya, na jamii kwa ujumla vinapaswa kushirikiana kuhakikisha kwamba wanawake wanapata ulinzi wa kutosha dhidi ya janga hili.


