Popular services

MTAZAMO WA DINI KUHUSU UZAZI WA MPANGO ZANZIBAR:UISLAMU NA UKRISTO WAPAZA SAUTI.



Na: Hamisi  Nishani – Zanzibar

Katika jamii za kisasa, suala la uzazi wa mpango limekuwa mjadala mkubwa, likihusisha haki na athari zake kwa familia na jamii kwa ujumla. Licha ya kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya jamii na taifa, dini nyingi duniani zina mitazamo tofauti kuhusu suala hili. Kila dini ina mafundisho yake kuhusu majukumu ya kifamilia, uzazi, na mipaka ya kupanga idadi ya watoto.Makala haya yanaangazia mtazamo wa dini ya Kiislamu na Ukristo kuhusu uzazi wa mpango visiwani Zanzibar.

Mtazamo wa Uislamu

Katika juhudi za kutoa mwanga juu ya suala hili, makala haya yalizungumza na Sheikh Abdalla Hamid Suleiman, mkufunzi wa Chuo cha Kiislamu Mazizini, Zanzibar, Sheikh Abdalla anasema kuwa Uislamu haukatazi uzazi wa mpango, kwani ni dini iliyokamilika katika nyanja zote.Kwa mujibu wa Qur’an, Mwenyezi Mungu anasisitiza umuhimu wa malezi bora. Ananukuu aya ya 233 ya Surat Al-Baqarah inayosema:"Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha na wazazi wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwa na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayoyatenda."

Sheikh Abdalla anaeleza kuwa hata Maswahaba wa Mtume walikuwa wakitumia njia za kiasili kama vile kumwaga mbegu nje, na Mtume hakuwahi kukataza jambo hilo.

Pia anabainisha kuwa Uislamu unasisitiza afya bora kwa mama na mtoto. Kupitia uzazi wa mpango, mtoto anapata malezi bora ya kiafya, mama anapata muda wa kupumzika, na baba anaweza kuwahudumia watoto kwa ufanisi zaidi.

"Afya ni neema kubwa kutoka kwa Allah na tunapaswa kuitunza," anasema Sheikh Abdalla, akinukuu Sahih Bukhari na hadithi nyingine katika Sunan Abu Dawood inayosema:"Hakuna madhara katika kutumia njia za kupanga uzazi, kama ni kwa ajili ya kumlinda mama au mtoto."Hata hivyo, Sheikh Abdalla anasisitiza kuwa Uislamu hauja halalisha njia zote za kisasa za uzazi wa mpango. Anasema"Njia za kisasa zinaweza kutumiwa ikiwa hazina madhara kwa afya ya mwanamke au mtoto. Kama zina madhara, ni bora kuepuka na kutumia njia salama."


Mwaka 2019, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilitoa tamko kuhusu uzazi wa mpango, likieleza masharti matano yanayokubalika Kiislamu Kulinda afya ya mama,Kulinda afya ya mtoto, Kuhakikisha haki za mtoto, Kuhakikisha haki za mama na Kuhakikisha malezi bora ya kifamilia.Tamko hilo limetolewa na baraza la maulamaa Bakwata katika semina ya viongozi wa Kiislamu jijini Tanga, chini ya ufadhili wa mradi wa Uzazi wa Mpango (AFP).
Mtazamo wa Ukristo

Kwa upande wa Ukristo, makala haya yalizungumza na Mchungaji Costino John Paulinge wa Kanisa la TEG, Mwembe Majogoo, Zanzibar.Amesema kuwa mtazamo wa Kikristo juu ya uzazi wa mpango unazua mjadala mkubwa, kwani madhehebu yanatofautiana.

Kanisa Katoliki, kwa mfano, linapinga njia za kisasa kama vile vidonge, sindano, na kondomu, kwa imani kwamba kila tendo la ndoa linapaswa kuwa na lengo la kuzaa.Kwa upande mwingine, madhehebu ya Kiprotestanti kama Waanglikana na Walutheri yanakubali uzazi wa mpango, wakiona kuwa ni njia ya kuhakikisha ustawi wa familia na afya ya mama.


Mchungaji Paulinge ananukuu 1 Timotheo 5:8, inayosema:"Ikiwa mtu hatunzi watu wa nyumbani mwake, amekataa imani na ni mbaya kuliko asiyeamini."Hii inasisitiza uwajibikaji wa kifamilia, jambo linalotafsiriwa na madhehebu fulani kama ruhusa ya kupanga uzazi kwa ajili ya ustawi wa familia.

Mchungaji anabainisha kuwa licha ya mgongano wa kimadhehebu, madhehebu ya Kisasa ya Kikristo yanakubali uzazi wa mpango kama sehemu ya maisha ya kisasa.

Mtazamo wa Kitaalamu

Dkt. Ummukulthum Omar Hamad, Daktari Bingwa wa Afya ya Uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, anaeleza umuhimu wa uzazi wa mpango katika afya ya jamii.Amesema kuwa uzazi wa mpango husaidia,Kulinda afya ya mama na mtoto,Kupunguza hatari ya magonjwa yanayohusiana na magozwa ya zinaa,kuboresha ustawi wa familia ,kupunguza hatari za mimba za mapema ,kukuza elimu na ufanisi wa kiuchumi na Kukuza haki za wanawake na usawa wa kijinsia.


 Fatma Haji Ali na Haule Costino John wanaeleza kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi."Wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya uzazi wa mpango, jambo linalopelekea madhara kiafya na kijamii. Ni muhimu taasisi za afya na vyombo vya habari kushirikiana kutoa elimu sahihi," wanasema.

Hitimisho

Mjadala wa uzazi wa mpango katika mtazamo wa dini unadhihirisha tofauti za kiimani na kijamii,Wakati Uislamu unaruhusu uzazi wa mpango kwa masharti fulani, Ukristo unatoa maoni tofauti kulingana na madhehebu.Kwa mtazamo wa afya, wataalamu wanasisitiza kuwa uzazi wa mpango una faida kubwa kwa ustawi wa familia na jamii. Elimu zaidi inahitajika ili kuwapa wananchi uelewa sahihi juu ya suala hili.