Popular services

DIWANI AKABIDHI FEDHA TASLIMU NA VIFAA VYA UJENZI KWA AJILI YA NYUMBA YA KATIBU WA UWT



Na: Nishan Khamis
Wilaya ya Kaskazini A, Unguja

Diwani wa viti maalum Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Bi Faida Salmin Juma, leo tarehe 26 Machi 2025, amekabidhi fedha taslimu na vifaa vya umeme kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wilaya hiyo. Hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Mwenyekiti wa UWT Taifa, Bi Merry Pius Chatanda, ambaye alisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba za watumishi wa UWT katika kila wilaya nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bi Faida alisema kuwa katika kuunga mkono ujenzi huo, ametoa mchango wa elfu tisini pamoja na kununua baadhi ya vifaa vya umeme. Alibainisha kuwa mchango huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maendeleo ya jumuiya hiyo na chama kwa ujumla.

Aidha, alisisitiza kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, hivyo akawahimiza wanachama kuhakikisha wanawapa kura za ndiyo marais wote wa nchi pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili chama hicho kiendelee kuongoza na kuleta maendeleo zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kaskazini A, Bi Lucy John Mpembo, alieleza kufurahishwa na mchango huo, akisema kuwa utawezesha kuendeleza ujenzi wa nyumba hiyo kwa mujibu wa agizo la Mwenyekiti wa UWT Taifa. Alisema ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa jumuiya hiyo na kuimarisha utendaji wao.

Aliongeza kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2025, na hivyo akatoa wito kwa viongozi, wajumbe na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango bora.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya UWT Wilaya hiyo, Bi Rahma Abdalla, alisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano katika kukamilisha ujenzi huo. Alitoa rai kwa wanachama, viongozi na wadau wa UWT kujitokeza na kuendelea kuchangia ili kufanikisha azma hiyo muhimu kwa ustawi wa jumuiya na chama.