Na: Nishan Khamis – Zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZANZIBAR kimewataka waandishi wa habari na watengenezaji wa maudhui ya mitandao ya kijamii kutumia majukwaa hayo kuhamasisha wanawake kuchangamkia fursa za uongozi, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Sofia Ngalapi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA-ZNZ, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa watengenezaji wa maudhui ya mitandaoni yaliyofanyika katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Ngalapi amesema taasisi hiyo itaendelea kufanya uchechemuzi wa kutetea haki za wanawake na watoto, huku ikiwataka wanahabari na watengenezaji wa maudhui kutumia taaluma yao kuandika habari chanya kuhusu wanawake, na kuwawezesha kufikia nafasi mbalimbali za uongozi kwa njia ya kuhamasisha na kutoa elimu.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo Bi. Salma Ali Saadat amesema mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, akisisitiza kuwa maudhui yanayozalishwa yazingatie ubunifu, utafiti wa kina, matumizi ya takwimu sahihi na kufuata misingi ya taaluma ili kuwa na athari chanya kwa wanawake.
Akihitimisha mafunzo hayo, Afisa Mawasiliano wa TAMWA-Zanzibar, Khairat Ali Haji, alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na SWIL unalenga kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi kupitia mitandao ya kijamii, na kuwahimiza washiriki kuzingatia mila, desturi na silka za Kizanzibari katika utekelezaji wa majukumu yao bila kuvuka mipaka ya utamaduni.
Washiriki wa mafunzo hayo walitoa shukrani kwa TAMWA-Zanzibar kwa fursa waliyoipata, na kuahidi kutumia maarifa waliyopata kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya kwa wanawake na taifa kwa ujumla.
